Tuesday, 9 July 2013

Komandoo Salmin atoa ya moyoni


Na Antar Sangali, Zanzibar
RAIS mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, amewaonya Wazanzibari kuacha pupa, badala yake watukuze uzalendo wakati wa mjadala wa kupata katiba mpya.
Amesema wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa yanapotokea machafuko.
Dk. Salmin, maarufu Komandoo, alitoa kauli hiyo juzi, alipohutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kibandamaiti, mjini Unguja.

Alisema harakati za ukombozi wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Afrika, hazipaswi kupuuzwa, na wachache kuachwa kuvuruga amani.
Dk. Salmin alisema wanawake walikuwa mstari wa mbele kubeba watoto migongoni usiku na mchana hadi uhuru ulipopatikana, hivyo hawastahili kurejeshwa kwenye zama hizo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, vijana katika taifa lolote ndiyo ngao ya amani, hivyo aliwahimiza kuendelea kusimama kidete kuilinda misingi ya Mapinduzi na Muungano.
Alisema ili kazi hiyo ifanikiwe, ni lazima wazee wakatimiza wajibu wao.
“Nimefarijika kwa kutembelewa na UVCCM nyumbani, niliyosema yametikisa dunia, niko tayari kuanza kujikongoja, naamini wazee wenzangu nao watafanya hivyo ili kutetea na kulinda misingi ya mapinduzi kwa nguvu na hekima,” alisema.
Dk. Salmin alisema nguvu na mchango wa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo iliyoviinua vyama vya TANU na ASP kuleta uhuru wa 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.
“Nami sasa sijambo, nipo tayari, umoja wetu utadumu, Chama chetu kitadumu, pia Afrika itaendelea kudumu, nitajikongoja pamoja nanyi kila nitakapotakiwa,” alisema Dk. Salmin, ambaye anasumbuliwa na matatizo ya macho.
Wakati Dk. Salmin akihutubia umati, vijana walipita na mabango yaliyoandikwa ‘kuweni macho na manyang’au wanaonyemelea kurudisha ukoloni’ ‘uhuru wa nchi hauji mara mbili’ ‘simameni imara kulinda mapinduzi kwa gharama yeyote’.
Maneno katika mabango hayo yalikariri vibwagizo vya Dk. Salmin alipokutana na ujumbe wa UVCCM nyumbani kwake, Migombani, mjini Unguja.
Wakati Dk. Salmin akihutubia jukwaani, mwanasiasa mkongwe Abdulrazaq Simai Kwacha na Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Fatma Karume, walikuwa wakimsiliza kwa makini, huku wakitingisha vichwa.
Kabla ya kupanda jukwaani, Dk. Salmin alitanguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, aliyewataka wanachama kuwa makini na baadhi ya wanasiasa wanaopotosha historia ya Mapinduzi na Muungano.
Ameir alisema Zanzibar imekumbwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa na maisha ya watu kupotea kwa ajili ya kupigania utu na heshima ya wanyonge, hivyo ni lazima Wazanzibari wakailinda hadhi hiyo ili isipotezwe na wapinga Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuia Ali Vuia, alisema Muungano umeleta tija, ikiwemo kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru