Tuesday, 16 July 2013

Tanzania kuuza umeme nje


NA SELINA WILSON
TANZANIA itajitosheleza kwa nishati ya umeme ifikapo mwakani, na kuuza ziada ya megawati 500 nje ya nchi.
Imeelezwa ifikapo mwaka 2015 megawati 1,500 zitauzwa nje na mwaka 2016 zitauzwa megawati 1,800, hivyo kuliingizia taifa mapato makubwa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema hayo baada ya kutiwa saini mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya China Power Investment Co Ltd (CPI).
Profesa Muhongo alisema malengo hayo yatafikiwa baada ya kukamilika ujenzi wa bomba kubwa la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.
Alisema wameanza kupokea mabomba kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo, na mikakati ni kuhakikisha ujenzi unakamilika katika muda uliopangwa kwa kuwa mahitaji ya gesi ni makubwa.
Waziri alisema sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo sita ya kipaumbele cha serikali, hivyo katika mpango wa kutekeleza miradi yenye matokeo makubwa (BRN), inakusudiwa kufikia uzalishaji wa megawati 3,000 ifikiapo mwaka 2015.
Profesa Muhongo alisema mauzo ya umeme nje yataiwezesha nchi kubadilisha bajeti na kuondokana na kutegemea mapato kutokana na viberiti na bidhaa zingine.
Aliwataka Watanzania waepuke kuweka vikwazo katika matumizi ya rasilimali zilizopatikana nchini, kwani kwa kufanya hivyo wanakwamisha ukuaji uchumi.
“Gesi ni rasilimali ya Watanzania, lazima itumike kuleta maendeleo ya wote. Wanaotaka isitumike wanachelewesha jitihada za kupeleka nchi katika uchumi wa kati.
“Itafika wakati itabidi tugawanyike makundi mawili, wanaotaka maendeleo wakae peke yao na wale wasiotaka wabaki kwenye kundi lao, ili tusikwamishane,” alisema.
Alisema kuna tatizo kubwa la ajira, hadi wengine wanaliita bomu linalosubiri kulipuka, ambalo utatuzi wake ni kuongeza viwanda na kufungua fursa za kibiashara, mambo yanayowezekana kama kutakuwa na umeme wa uhakika.
Profesa Muhongo alisema umeme ukizalishwa kwa wingi, viwanda vingi vitajengwa na kuwezesha vijana kupata ajira, huku uzalishaji bidhaa ukiongezeka maradufu na kuuzwa nje.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alisema Tanzania inateswa na mfumuko wa bei kila wakati kutokana na kutegemea bidhaa nyingi kutoka nje.
Alisema utegemezi huo unatokana na kushindwa kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa kwa sababu ya ukosefu wa nishati ya uhakika na ya kutosha.
Balozi huyo alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete, za kuzalisha umeme wa kutosha, anaamini Tanzania itaondokana na tatizo hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru