Tuesday, 9 July 2013

Dk. Sheni aonya wafanyabiashara


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema haitavumilia kuona watu wanahatarisha maisha na afya za wengine, hususan wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Hatari hiyo ni kwa kuwauzia bidhaa zilizopitwa na wakati, mbovu, bei ya juu na zisizokuwa na vipimo bora.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari, Rais Dk. Ali Mohammed Sheni, alisema hayo jana katika risala ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani, aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Dk. Sheni alisema wakati watu wanatafuta riziki katika mwezi huu, wanapaswa kuzingatia haki na kurehemiana katika biashara.
Alisema inafahamika kuwa faida kwa mfanyabiashara ni lazima ili aweze kujimudu na kuendelea, lakini wakati huo huo akumbuke kufanya biashara bila hadaa.
Dk. Sheni aliviagiza vyombo husika kuchukua hatua madhubuti kuhusu masuala ya biashara na mazao ya kilimo, kama vile ndizi zinazouzwa sokoni zikiwa changa.
Aliwataka wananchi kurehemiana kwa njia mbalimbali, hususan kutoa sadaka kwa kuwasaidia wasiojiweza, yatima, masikini, wanafunzi, wagonjwa na watu wengine wanaohitaji kusaidiwa.
Dk. Sheni alisema mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekuja wakati wa msimu wa utalii, hivyo ni vyema kuwaongoza wageni kwa utaratibu, mila na kanuni zilizopo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru