Monday, 8 July 2013


Mgawanyo mkoa wa Mbeya wazua tafrani
NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MAPENDEKEZO ya kuugawa mkoa wa Mbeya, yamezua tafrani, ambapo baadhi ya vigogo wametofautiana na Mkuu wa mkoa huo, Abbas Kandoro.
Kutokana na hilo, baadhi wameanza kumtisha Kandoro na kudai watafanya maandamano ili kuhakikisha anang’olewa mkoani humo.
Baadhi wanamtuhumu mkuu huyo wa mkoa kwamba amekula rushwa ili kufanikisha kuanzishwa mkoa mpya wa Songwe.
Hata hivyo, Kandoro amesema hafanyi kazi kwa vitisho vya mtu, bali kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu.
Kandoro akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema ameanza kutishwa baada ya mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kuugawa mkoa wa Mbeya na kupata mpya wa Songwe, utakaokuwa na makao makuu Mkwajuni.
Alisema anashangazwa na madai yanayotolewa kwamba amekula rushwa ili kuufanya Songwe kuwa mkoa mpya, na kuhoji rushwa hiyo ni ya shilingi ngapi?
Kandoro amesema hana mpango wa kugombea ubunge mkoani Mbeya, hivyo hawezi kufanya upendeleo wowote katika hilo, bali vigezo ndivyo vilivyopewa kipaumbele.
“Ni vyema watu hawa wangeelewa sikufukuzwa kwetu, nimekuja Mbeya kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo sifanyi kazi kwa vitisho vya mtu bali kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu,” alisema.
Alisema serikali haiwezi kuacha kuwasogezea wananchi huduma kwa sababu ni wachache, bali watajumlishwa na walio wengi ili kuwapatia huduma za msingi zinazohitajika.
Kandoro alisema wapo watu walioanza kutoa kauli za ajabu baada ya RCC kupendekeza mkoa mpya utakaoanzishwa baada ya kuugawa wa Mbeya, uitwe Songwe, utakaokuwa na wilaya za Ileje, Mbozi, Momba na Chunya.
Kwa mujibu wa Kandoro, watu hao wamefikia hatua ya kusema wataandamana ili kuhakikisha anaondolewa mkoani humo.
Alisema ni vyema ambao hawajaridhika na uamuzi wa RCC watambue bado kuna nafasi ya kufikisha fikra zao kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kugawa nchi katika maeneo ya utawala.
Kandoro alisema badala ya kukimbilia kufanya maandamano barabarani na kufanya fujo kwa lengo la kupambana na Kandoro, ni vizuri wajenge hoja za msingi na kuzipeleka kwa Rais Kikwete, na kueleza kwa nini wanafikiri uamuzi wa RCC si wa busara.
Aliwaomba wananchi kuwa watulivu, wenye kuvuta subira na wanaojenga hoja. Alisema  iwapo wana jambo linalowatatiza watafute utaratibu mzuri wa kufikisha fikra zao na si kufanya fujo.
Mkuu wa mkoa alisema uamuzi wa kuugawa mkoa wa Mbeya na kupatikana mpya wa Songwe haukuwa wake, bali unatokana na mahitaji ya wana-Mbeya wenyewe, ambao wamekuwa nao kwa miaka mingi.
Alisema miaka ya nyuma kulikuwa na kikao kilichojulikana Kamati ya Maendeleo ya Mkoa (RDC), ambacho kiliwahi kujadili kuugawa mkoa, ambapo mapendekezo yalitolewa ambayo hayakufika mbali kutokana na mivutano iliyojitokeza.
“Hili jambo lililofikiwa na RCC si jipya, lilikuwepo siku nyingi mioyoni mwa wana-Mbeya na halikuanzishwa na Kandoro,” alisema.
Alisema wapo watu wanaoiangalia Chunya kwa sura ya maeneo ya Mkwajuni, Chunya mjini au Makongolosi, lakini wanasahau kuna maeneo ya Ngwala au Gua, ambayo nayo ni sehemu ya Chunya.
Kandoro alisema jambo la kuugawa mkoa wa Mbeya linatokana na mahitaji maalumu  ya kuyafanya maeneo mengine yasogezewe huduma ili kuchochea maendeleo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru