Friday, 12 July 2013

Stars kanyaga twende


NA ATHANAS KAZIGE
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa, ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen, amesema mchezo wa leo dhidi ya Uganda utakuwa mgumu lakini ushindi ni lazima. Taifa Stars na Uganda ‘The Cranes’ zinajitupa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kuwania kushiriki Fainali za Kombe la CHAN.
Kim, alisema amewapa mazoezi ya kutosha wachezaji wake ili kuikabili vyema Uganda, ingawa amekiri kuwa mchezo utakuwa na changamoto kubwa. Akizungumza Dar es Salaam jana, Kim alisema wamejipanga vyema kushinda mchezo huo unaotarajia kuwa na msisimko.
Alisema kuwa vijana wake wana afya njema na hakuna majeruhi, hivyo ana matumaini watacheza kwa kufuata mafunzo yake.
Kim, alisema wachezaji wana ari kubwa ya ushindi baada ya kuonyesha uwezo katika mazoezi ya kikosi hicho.
“Najua wazi mchezo wa kesho (leo) utakuwa mgumu sana, lakini vijana wangu nimewapa mafunzo ya kutosha. Wameonekana wana uwezo mkubwa katika mazoezi naomba mashabiki waje kwa wingi,” alisema Kim.
Alisema ushindi wa leo utakuwa chachu ya kufanya vyema katika mechi ya marudiano itakayochezwa mjini Kampala Julai 27, mwaka huu. Kocha Mkuu wa Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ alisema anatambua Uganda inapambana na timu ngumu ya Taifa Stars iliyosheheni wachezaji mahiri.
Fainali za CHAN zimepangwa kufanyika nchini Afrika Kusini. Taifa Stars inavaana na Uganda, baada ya kulala mabao 3-2 na Ivory Coast katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru