Friday, 19 July 2013

Katibu Mkuu Ardhi apanda kizimbani


NA FURAHA OMARY
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, ameieleza mahakama kuwa, sh. milioni 100 zilihamishwa kutoka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi, kwenda wizarani kinyume cha utaratibu.
Rutabanzibwa alidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alipotoa ushahidi katika kesi inayowakabili waliokuwa Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Simon Lazaro, Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Gerald Mango na Kaimu Mhasibu Mkuu, Charles Kijumbe.
Mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, alidai hajui kama fedha hizo zimeibwa, kwani hazijulikani zilivyotumika.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, kutoa ushahidi Rutabanzibwa alidai mwishoni mwa mwaka wa fedha 2010/2011, Mango aliomba sh. milioni 200 kwa ajili ya mipango bora ya matumizi ya ardhi, kwa msingi wa dharura.
Rutabanzibwa alidai mkurugenzi huyo aliandika barua kwa katibu mkuu wa wizara, ambapo alimwelekeza kaimu mkurugenzi wa sera na mipango ashughulikie hilo kwa kuomba fedha HAZINA, ambazo zilikuwa nje ya bajeti.
Alidai fedha zilizoombwa zilikuwa kwa ajili ya mipango ya dharura katika matumizi ya ardhi katika wilaya tano.
Shahidi huyo alidai hana uhakika wa jinsi zilivyotumika, lakini aliambiwa sh. milioni 100 zilirejeshwa wizarani na kukabidhiwa kwa Lazaro, ambaye ni mshitakiwa katika kesi hiyo.
“Baada ya mwaka mmoja tulielezwa na TAKUKURU kuwa kuna tatizo la matumizi mabaya ya fedha. Lazaro na Mango walinieleza fedha hizo zimerejeshwa wizarani na kwamba, Lazaro alitia saini stakabadhi tatu kueleza amepokea sh. milioni 100 na kumkabidhi mhasibu.
“Stakabadhi zilikuwa zinasema Lazaro anakiri kupokea sh. milioni 100 kwa tarehe tofauti ambazo zilikuwa kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi ya wizara,” alidai.
Katibu mkuu alidai alichogundua katika fedha hizo ni kwamba, hazikuombwa kwa maandishi kutoka tume kwenda wizarani na zilipelekwa kinyume cha utaratibu wa kuhamisha fedha za serikali.
Alidai tume ilitakiwa kuandika hundi kwenda wizarani, ambako zingeingizwa kwenye akaunti ndipo zitumike kama ilivyokusudiwa.
“Kazi iliyokuwa ifanyike kwa mujibu wa stakabadhi ni tofauti na kazi iliyoombwa ya sh. milioni 200. Stakabadhi za sh. milioni 100 ni za kienyeji za Lazaro, ambazo alizifanyia marejesho ya masurufu zilizokuwa za kazi iliyokuwa na bajeti yake katika wizara,” alidai.
Sehemu ya ushahidi wa Rutabanzibwa akihojiwa na mawakili wa utetezi Henry Massaba na Msemwa ni kama ifuatavyo:
Massaba: Kosa la Mango ni nini, alichukua fedha na kumkabidhi Lazaro?
Shahidi: Hawezi kutueleza hizo fedha zilipelekwa kwa Lazaro kwa kitu gani kama kanuni zinavyosema.
Massaba: Anatakiwa na nani kueleza hilo?
Shahidi: Sheria na vifungu mbalimbali na kwamba, nyaraka za serikali hazikutumika katika kuhamisha fedha hizo.
Massaba: Katika ushahidi wako, Mango ana kosa gani?
Shahidi: Ametoa sh. milioni 100 kwa matumizi ambayo hayaeleweki na kinyume cha matumizi ya fedha za serikali.
Msemwa: Fedha ziliibiwa au?
Shahidi: Usiniingize huko. Sijui kama zimeibwa, kwani hazijulikani zilivyotumika na zimekwenda kinyume cha sheria.
Kesi hiyo itatajwa Agosti 15 na  itaendelea kusikilizwa Septemba 2 na 3, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Lazaro anadaiwa kuwa Mei 18, 2012, katika ofisi za tume hiyo, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa na wadhifa huo kwa nia ovu aliwasilisha nyaraka za marejesho kwa Mkurugenzi wa tume, kuonyesha alipokea sh. milioni 100 kutoka tume, kwa ajili ya mipango ya ardhi wilaya za Babati, Kilolo na Bariadi, huku akijua si kweli.
Lazaro, Mango na Kijumbe wanadaiwa kati ya Julai 4, na Agosti 5, 2011, Ilala, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa nia ovu walitumia madaraka yao vibaya.
Katika shitaka lingine, Lazaro anadaiwa tarehe tofauti kati ya Julai 4 na Agosti 5, 2011, Dar es Salaam, kwa kujua alibadilisha  matumizi ya sh. milioni 100 alizopewa na tume kwa ajili ya mipango ya ardhi katika wilaya za Arusha, Muleba, Ngorongoro, Songea, Kilosa na Mpanda.
Katika shitaka la nne, akiwa mtumishi wa umma, Lazaro anadaiwa katika tarehe hizo, wilayani Ilala, aliiba sh. milioni 100 alizoaminiwa na tume kwa ajili ya matumizi ya mipango ya ardhi katika wilaya hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru