Tuesday, 2 July 2013

JK: Tuchangamkie matumizi ya sayansi na teknolojia


Na Hamis Shimye  
RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kujipanga kisawasawa katika kuharakisha matumizi ya sayansi na teknolojia ili kusaidia kujiletea maendeleo binafsi na nchi.
 Pia, amesema anashangazwa na watu wanaoendelea kupiga kelele juu ya siasa kila siku, huku wakishindwa kuzungumzia mambo muhimu kuhusiana na changamoto juu maendeleo ya sayansi na teknolojia.
 Rais Kikwete alitoa wito huo juzi usiku wakati akifunga mkutano wa Majadiliano ya Pamoja kwa Manufaa ya Wote - Smart Partnership Diaologue katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
 Alisema maendeleo hayawezi kuja kama hapatakuwa na uharaka wa matumizi ya sayansi na teknolojia, kwa kuwa ukiwa nyuma kiteknolojia huwezi kufanikiwa kwa jambo lolote.
Tukazane, tujiwekee malengo yetu kwa kuwa nchi zilizofanikiwa zimefika huko kutokana na kuwekeza katika teknolojia ambayo imeweza kuwaletea maendeleo muhimu,” alisema.
Alisema tangu kuanza kwa majadiliano hayo mwaka 1995, kumeonekana kuwa kuna umuhimu mkubwa wa uwekezaji na matumizi ya sayansi na teknolojia katika kuharakisha maendeleo.
 Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Msumbiji, Joackim Chisano alisema kupitia majadiliano hayo ana uhakika kila mmoja ataweza kukabiliana na changamoto zinazomkabili kwa upande wa sayansi na teknolojia katika nchi yake.
 Katika hatua nyingine, majadiliano hayo yalihitimishwa rasmi jana, ambapo sekretarieti ya mdahalo huo iliamua mambo mbalimbali, ikiwemo ya kuzitaka nchi za Afrika kuwekeza na kutoa fursa kwa vijana katika nyanja hiyo.
 Majadiliano hayo yaliyofanyika kwa siku tatu yalimalizika juzi na yanatarajia kufanyika mwakani nchini Afrika Kusini kwa baadhi ya viongozi wa Afrika na Asia kukutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo katika sayansi na teknolojia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru