Monday, 15 July 2013

Mbowe ajisalimisha polisi


Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amejisalimisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kutokana na tuhuma zinazomkabili, zikiwemo kauli za uchochezi dhidi ya jeshi hilo, vyombo vingine vya dola na serikali kwa jumla.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, mwenyekiti huyo alijisalimisha jana mchana.
Advera alisema polisi inaendelea kumhoji Mbowe kuhusu kauli hizo za uchochezi na kuijengea jamii taswira mbaya kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama na kuwafanya wananchi kuwa na hofu.
Kwa mujibu wa Advera, uchunguzi wa kina unaendelea na itakapothibitika kuhusika kwake au mtu mwingine yeyote kutoka ndani au nje ya CHADEMA hatua za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Wakati Mbowe akijisalimisha, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeionya CHADEMA na vyama vingine vinavyofikiria au kutaka kuanzisha vikundi vya ulinzi.
Imeitaka CHADEMA kuacha mara moja mpango huo na kwamba, atakayekaidi atachukuliwa hatua kali za kisheria, ambazo hazitaweza kukatiwa rufani katika mahakama yoyote.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo, Uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ni wa mwisho.
Tamko hilo lilitolewa jana kupitia taarifa kwa vyombo vya habari baada ya CHADEMA kutangaza kuanzisha kambi ya mafunzo kwa kikundi chake cha vijana cha ‘Red Brigede’.
Mafunzo hayo yalitangazwa mbele ya waandishi wa habari na Mbowe, ikiwa ni moja ya maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
Mbowe alisema uamuzi huo umefikiwa ili kuwapa mbinu vijana hao za kukilinda chama hicho na viongozi wake, kwa madai kuwa wanaonewa na polisi.
Kauli ya Mbowe iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa chama hicho, Singo Kigaila, aliyesema mafunzo hayo yataanza wiki hii, na hakuna mtu yeyote atakayewazuia kufanya hilo.
Jeshi la Polisi kwa mara kadhaa lilitoa tamko kuionya CHADEMA kuacha mpango huo, likisema yeyote atakayehusika kufadhili, kuwahifadhi na kuwakusanya vijana atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Rajab Juma, kwa niaba ya Tendwa, ofisi ya msajili imeelezea kusikitishwa na kauli ya Mbowe kuhusu uanzishwaji wa kikundi hicho bila kuwasiliana na ofisi hiyo.
“Ofisi ya msajili inashangazwa na uamuzi huu, awali CHADEMA ilishawahi kutaka kuanzisha kikundi kama hiki na kuelezwa ni kukiuka sheria ikaacha kufanya hivyo,’’ ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema wakati huo, CHADEMA iliandikiwa barua kwa msajili yenye kumbukumbu namba RPP/CHADEMA/72/29 ya Desemba 31, mwaka 2004.
Imeelezwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa barua yenye kumbukumbu namba CAB/208/208/353/03/2 ya Desemba 29, mwaka 2004, ilielezwa kufanya mafunzo ya kujilinda ni kukiuka sheria za nchi.
Ofisi hiyo ilisema mwaka 2004 CUF iliandika barua kwa msajili ikitaka maelezo juu ya kuanzishwa kwa kikundi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CUF iliandika barua kwa msajili yenye kumbukumbu namba CUF/Ak/DSM/RPP/0034/7G/2004/14 Aprili 3, mwaka 2004
iliyoandikwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wilfred Lwakatare, kumtaarifu na kuomba ufafanuzi kutoka kwa msajili kuhusu kikundi hicho.
Katika majibu ya msajili kwa CUF, kupitia barua yenye kumbukumbu namba RPP/CUF/77/42 ya Mei 15, mwaka 2004, ilielezwa kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pia aliwaelewesha CUF kuhusu suala hilo na kupiga marufuku mpango huo kwa barua yenye kumbukumbu namba AB 286/386/353/01/73.
Kutokana na hilo, ofisi hiyo  imesisitiza kwamba, sheria zinazokataza suala hilo hazijabadilika na viongozi wa CHADEMA ni wale wale walioonekana kuelewa na waliositisha kutekeleza mpango huo mwaka 2004.
“Nia ya CHADEMA haieleweki. Kama ni kupima matokeo iwapo watatekeleza mpango huu, basi uamuzi wao hautakuwa wa busara kwa uhai wa chama chao.
“Kuendelea kufanya mafunzo kwa chama ni kukiuka sheria za nchi, ikiwamo ya vyama vya siasa ya 1992 kifungu 9(2)(c), ambacho kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu na vurugu ili kufikia malengo yake ya kisiasa,” alisema.
Ofisi hiyo imesema msajili atachukua hatua kali za kisheria kwa chama kitakachoshindwa kutii agizo hilo, kwa kuwa kifungu cha 19 kinatoa mamlaka ya kukifuta chama kinachokiuka masharti ya usajili na kifungu cha 20 kinaeleza uamuzi wa msajili ni wa mwisho.
UFAFANUZI KATIBA ZA VYAMA
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, ofisi ya msajili ilishatoa ufafanuzi mwaka 2004, wakati vyama vya siasa vilipoandika barua kutaka kuanzisha vikundi hivyo kwa kuwa katiba za vyama vyao zinaruhusu.
“Ufafanuzi tuliotoa ni kwamba, vikundi hivi ni wanachama wanaopewa jukumu na chama kuangalia usalama wa mali na viongozi wa chama.
“Hili ni kama ambavyo majumbani tunaangalia au tunaweka watu wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au ukakamavu kuangalia usalama wa nyumba zetu mchana hata usiku,’’ ilisema taarifa hiyo.
Katiba ya nchi imempa jukumu kila mwananchi kulinda amani na usalama, pia kujilinda yeye na mali zake, kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale anaposikia au kuona mtu anataka au anafanya uhalifu au anataka kumdhuru.
Taarifa hiyo ilisema katiba ya nchi au katiba za vyama hazina maana ya kila mwananchi au kikundi fulani kifanye mafunzo ya kijeshi au ukakamavu ili kufanikisha jukumu  hilo.
Alisema vinapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola na si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kwa kuwa, wenye jukumu la ulinzi ni vyombo vya ulinzi na usalama.
USHAHIDI JUU YA CCM
Taarifa hiyo ilisema madai kuwa CCM ina kambi za mafunzo ya vijana kupambana ni kisingizio cha kuvunja sheria na hayana msingi.
Imeviasa vyama vya siasa kutumia muda wake kufanya siasa ili kuchangia maendeleo, badala ya kubuni mambo yanayoleta mtafaruku.
Ofisi hiyo ilisema amani ikitoweka vyama vya siasa vitakuwa katika makaratasi, hakutakuwa na mikutano ya vyama, kamati kuu, mkutano wa waandishi wa habari au operesheni kwa kuwa demokrasia hutekelezwa na kukua mahali penye amani na utulivu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru