Wednesday 10 July 2013

Waziri wa ardhi atoa onyo kali


 NA MARCO KANANI, GEITA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametoa onyo kali dhidi ya watu wanaoshirikiana na watumishi wa umma kujimilikisha kiharamu maeneo ya shule, kuwa hatakuwa na huruma nao.

Waziri Anne aliyasema hayo jana mkoani hapa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kalangalala na kuhuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Msukuma Kasheku, alipomweleza waziri huyo kwamba  kuna watu wamejigawia maeneo ya shule ya msingi Nyankumbu iliyo katika mji wa Geita.
Profesa Anne, alionekana kukerwa na  kitendo hicho na kutoa kauli kuwa maeneo ya shule yanapaswa kuheshimiwa na marufuu kuyavamiwa ama kupewa watu kwa shughuli zao nyingine tofauti na za kielimu.
Alisema iwapo watu hao walishapewa hati miliki, atahakikisha wanafutiwa, kwani inawezekana walizipata kwa njia isiyo halali.
Waziri huyo, alitoa onyo kwa watumishi wa Idara ya Ardhi wanaoshirikiana na watu hao kufanya uporaji wa maeneo muhimu ya shule.
Aliwataka kuacha uovu huo kabla ya hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.
Aidha, katika mkutano huo, alisema serikali ina nia ya kuupanga mji wa Geita na watakapoanza, watoe ushirikiano.
“Tunataka Geita iwe na mji uliopangwa kitaalamu na baadhi ya nyumba zitalazimika kuvunjwa,” alisema Profesa Anne.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru