Wednesday 3 July 2013

Mossy: Wazazi washiriki kumwinua mtoto wa kike


Na Samson Chacha, Tarime
KAMPENI za kupinga unyanyasaji kwa wanawake na watoto wa kike nchini, zimeendelea kuungwa mkono kutokana na kujikita zaidi katika kusaidia jamii.Tayari taasisi mbalimbali zimejitokeza kuunga mkono kampeni hizo zinazoendeshwa na Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group (NkMG), ambapo sasa Umoja wa Waandishi wa Habari Wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, zimeahidi kuunga mkono katika kuhabarisha jamii.
Msimamo huo umetolewa jana wakati wa kikao baina ya Umoja huo wa wanahabari na Mkurugenzi Mtendaji wa Nyumbani Kwanza Media Group, Mossy Magere, kilichofanyika mjini ambapo, waliahidi kushiriki katika kuhamasisha na kuhabari jamii.
Mbali na kampeni za kupinga unyanyasaji ambazo zimezinduliwa Machhi 3, mwaka huu, wilayani hapa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, pia harakati mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wazazi na wahisani kuchangia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike, zimekuwa kiendeshwa kupitia kampuni hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuwaondolea watoto wa kike changamoto zinazowakabili ikiwemo mimba, utoro na wengine kutumikishwa kufanya kazi za majumbani na kwenye machimbo ya dhahabu.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa umoja wa wanahabari hao, Mossy alisema kwa sasa NkMG wanaendesha harambee kwa ajili ya ujenzi wa ,mabweni katika shule mbalimbali wilayani Tarime.
Amesema wanafunzi wa kike wamekuwa wakinyanyasika na kukosa haki za msingi kutokana na kukosekana kwa mabweni na kwamba, jamii inapaswa kuamka ili kuwakomboa na kutengeza kikazi bora.
"Ni lazima tuwalinde watoto wa kike ili wapate haki zao za msingi, tunajitaji kuunganisha nguvu katika hili. Kwa sasa tunafanya harambee kuchangia ujenzi wa mabweni kwenye sekondari zetu hapa Tarime na baadaye tutakwenda maeneo mengine,” alisema Mossy.
Alisema shule nyingi ambazo hazina mabweni wanafunzi wa kike wamekuwa kwenye hatari kubwa ikiwemo kutumikishwa, kubakwa na wengine kuwekwa vimada, jambo linalowafanya kukosa elimu.
Kuhusu harambee hiyo, Mossy aliwahimiza wazazi na walezu kujitokeza kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha sekondari ya Ingwe iliyopo Nyamongo inakuwa na mabweni kwa ajili ya watoto wa kike.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Tarime Press Club, Samson Chacha, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema, wameunga mkono jitihada hizo za Mossy na kwamba, watakuwa naye bega kwa bega ili kuhakikisha motto wa kike Tanzania anakombolewa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru