NA MWANDISHI MAALUMU
RAIS Jakaya Kikwete, amesema jukumu kubwa la gesi asilia ni kuwatoa Watanzania katika umasikini.
Amesema lazima wananchi waone na kuthibitisha manufaa ya gesi kwa maendeleo yao katika kipindi kifupi.
Rais amesema uchochezi wa baadhi ya wanasiasa kuhusu gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni changamoto, ambayo serikali iko tayari kupambana nayo.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na Mtendaji Mkuu wa Kundi la Kampuni za British Gas (BG), Chris Finlayson, Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ni miongoni mwa zilizogundua gesi na zimeanza kuwekeza katika uchimbaji wa rasilimali hiyo.
“Ni lazima gesi iwatoe watu katika umasikini na ibadilishe maisha yao, hivyo maandalizi ya uchimbaji yasichukue muda mrefu. Wananchi wanahitaji kuona manufaa ya gesi katika kipindi kifupi iwezekanavyo,” alisema.
Aliongeza: “Ni dhahiri ninyi wabia mtanufaika na gesi asilia kutokana na uwekezaji, lakini kimsingi wanataka iwanufaishe watu, iwatoe katika umasikini.”
Akizungumzia wanasiasa wanaowachochea wananchi wa Mtwara kudai gesi isitoke mkoani humo alisema:
“Uchochezi wa wanasiasa ni changamoto ambayo serikali itapambana nayo na ina uwezo wa kutosha wa kuimaliza.”
Finlayson alimweleza rais maendeleo ya maandalizi ya uchimbaji wa gesi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa Kitanzania kusomea utaalamu wa gesi.
0000
Muhula kidato cha tano wabadilishwa
NA RABIA BAKARI
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebadili muhula wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha tano.
Wanafunzi hao waliotakiwa kuingia darasani Mei, mwaka huu, sasa wataanza rasmi masomo Julai 15, mwaka huu.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philip Mulugo, alisema jana kuwa, wanafunzi hao wataanza masomo wiki ya tatu ya Julai, ambayo inaanza tarehe 15.
Alisema majina ya wanafunzi hao yatatangazwa hivi karibuni na yatawekwa kwenye vyombo vya habari.
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, alipotangaza matokeo mapya ya kidato cha nne Mei, mwaka huu, alisema majina ya watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa mapema ili wapate muda wa kujiandaa kuripoti shuleni.
Mulugo alisema kuchelewa kutangazwa majina hayo si tatizo, kwani wanafunzi wengi wanajua alama zao, na kikubwa wanachosubiri ni kupangiwa shule.
Kwa kawaida wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu, huku waliopata daraja la nne hadi pointi 28 hupangiwa vyuo mbalimbali, vikiwemo ya ualimu.
Tuesday, 9 July 2013
JK: Gesi iwaondolee wananchi umasikini
09:22
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru