Wednesday 3 July 2013

Tanzania yaongoza kwa saratani


NA MWANDISHI WETU

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ya shingo ya kizazi katika nchi za Afrika Mashariki.
Kikwete aliyasema haya juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa siku mbili wa wake wa Marais wa Bara la Afrika uliomalizika jana, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Alisema serikali ya Tanzania inaamini kuwa uchumi wa taifa unakuwa kufuatia watu wenye afya kujihusisha katika shughuli za kuongeza kipato.
Hata hivyo, alisema wamejipanga kukabiliana na magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa malaria na ukimwi.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, katika kukabiliana na hilo, wameanza kutekeleza mpango wa miaka mitano ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete alimshukuru Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush, kwa kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo.
Naye, Rais Bush, alisema ataunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya Rais kikwete katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema ufadhili huo umechangiwa na uhusiano wa muda mrefu baina yao.
Katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria, wataweka mipango ya muda mrefu.
Hata hivyo, Mke wa Rais wa Zambia, Dk. Christine Kaseba, alipongezwa na Rais Bush kwa kuanzisha taasisi ya kupambana na magonjwa ya saratani nchini kwake.
Pia, alilipongeza Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa (UNAID), kwa misaada inayosaidia nyanja mbalimbali nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru