Na Selina Wilson
RAIS Barack Obama wa Marekani, ameondoka nchini jana mchana kurejea nyumbani, baada ya kuhitimisha ziara ya kihistoria ya siku mbili, ambapo ameacha neema ya umeme.
Obama aliwasili jijini Dar es Salaam, juzi, saa 8.37 mchana na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, ambaye jana alimsindikiza kupanda ndege yake, Air Force One kurudi Marekani.
Kiongozi huyo wa taifa kubwa na lenye nguvu kiuchumi na kijeshi duniani, alifuatana na familia yake, mkewe Michelle na watoto Malia na Sasha, ambao walilakiwa na umati wa Watanzania.
Rais Obama ambaye muda wote wa ziara alionekana mwenye furaha, alikuwa akisalimiana na kucheka na watu kabla ya kukiri kuwa anajihisi yuko nyumbani.
Kupitia mradi huo, nchi hizo zitapata nishati hiyo mara mbili zaidi ya kiasi kilichopo, lengo likiwa kusaidia kuharakisha maendeleo.
Uzinduzi huo ni utekelezaji wa sera mpya ya Marekani kwa nchi za Afrika, katika kuziwezesha kuboresha sekta ya nishati. Mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji hadi kufikia megawati 10,000.
Rais Obama alizindua mradi huo jana, Ubungo, Dar es Salaam, kwenye mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi katika kituo cha Kampuni ya Symbion kutoka Marekani.
Katika hotuba ya uzinduzi, Rais Obama alisema anaamini mradi huo utatekelezwa kwa mafanikio, kwani ana matumaini makubwa na utendaji wa Rais Jakaya Kikwete na serikali yake.
Alisema kwa kuanzia, mradi huo utatekelezwa katika nchi sita za Afrika, Tanzania ikiwa ya kwanza kwenye orodha.
Rais Obama aliyekuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, alisema lengo ni kuwafikia watu milioni 20 barani Afrika.
Ili kutekeleza mradi huo, Rais Obama alisema serikali ya Marekani imetenga dola bilioni saba (takriban sh. trilioni 11.2), ambapo sekta binafsi nchini humo imetenga dola bilioni tisa (sawa na sh. trilioni 14.4).
Hata hivyo, alitaka jitihada ziongezwe katika usimamizi wa miradi ili ikamilishwe kwa wakati, kwa kuwa kuna changamoto ya ucheleweshaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema ni vyema miradi inayowagusa wananchi, hususan vijijini ikakamilishwa kwa wakati ili kuharakisha maendeleo na kuwafanya waishi maisha bora.
“Tunahitaji idadi kubwa zaidi ya Waafrika watumie umeme, ndiyo maana tumelenga kufikia watumiaji milioni 20. Umeme ukifika vijijini kutakuwa na uhakika wa maendeleo.
“Wafanyabiashara na wenye viwanda wapate umeme wa uhakika ili kuendesha shughuli zao bila changamoto ya kukosa nishati hiyo,” alisema.
Rais Obama alisema mabadiliko ya kimaendeleo katika ukuaji uchumi barani Afrika yatachochewa na uhakika katika uzalishaji umeme.
Alisema serikali ya Marekani imejizatiti ili kuhakikisha nchi za Afrika zinafungua fursa za kuboresha sekta za viwanda na biashara kwa kuzalisha zaidi na kuuza nje.
Rais Obama alisema jambo muhimu ni kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji miradi ya uzalishaji umeme, kwani Marekani imefanikiwa kwa kuishirikisha sekta hiyo.
Alisema nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha urafiki uliodumu kwa muda mrefu.
“Marekani imeisaidia Tanzania katika maeneo mengi, ikiwemo kupambana na malaria na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi. Pia katika sekta za elimu na kilimo kupitia mpango wa Feed the Future,” alisema.
MPIRA WA NISHATI
Kabla ya uzinduzi huyo, Obama na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete, walionyeshwa mipira miwili ya gesi, ambayo inaweza kutumika kuzalisha nishati ya kuwasha taa na kuchaji simu. Mipira hiyo inapochezwa ndipo inapozalisha nishati.
Mipira hiyo ni teknolojia iliyobuniwa na vijana wenye miaka 25, Jessica Matheus, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Uncharted Play Inc na Victor Angel, ambaye ni Makamu wa Rais wa kampuni hiyo.
Obama alirushiana mpira na Rais Kikwete ili kuongeza uzalishaji nishati na baadaye kufanya majaribio kwa kuwasha tochi na kuchaji simu.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo kwa Tanzania, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema sera mpya ya Marekani kuhusu nishati kwa bara la Afrika ni mpango mzuri.
Profesa Muhongo alisema wizara imejipanga vyema na imelenga kuboresha umeme vijijini na mijini, ambapo uzalishaji utaongezeka kutoka megawati 1,438.24 na ifikapo 2015 utaongeza mara mbili.
“Tunataka tufikishe megawati 2,880, lengo hasa ni kufikisha megawati 3,000, hivyo kitendo cha Marekani kupanga kuboresha sekta hiyo barani Afrika ni kuunga mkono jitihada za serikali,” alisema.
Alisema katika ziara ya Rais Obama, walifanya mazungumzo kuhusu mradi wa kuzalisha megawati 400 kutokana na gesi mkoani Mtwara, unaotekelezwa na Symbion na General Electric, ambapo sasa zitazalishwa megawati 600.
“Ziara hii imetusaidia, naamini hata wananchi wa Mtwara watafurahi zaidi kutokana na Symbion kuongeza megawati 200,” alisema.
Katika eneo la Ubungo, ulinzi uliimarishwa huku baadhi ya makachero wakilazimika kupanda juu ya ghorofa la makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kwenye mitambo ya Symbion ili kuhakikisha usalama.
Umati ulifurika katika Barabara ya Morogoro ambayo ilifungwa kwa ajili ya msafara wa Rais Obama. Kati yao walikuwa wakifuatilia uzinduzi huo na wengine wakitembea kwa miguu.
DONDOO KUHUSU SYMBION
Symbion yenye makao makuu Washington D.C, ndiyo inasimamia ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa na serikali ya Marekani.
Kwa kipindi cha miaka mitano ijayo imepewa jukumu la kutekeleza miradi ya umeme itakayowekezwa na serikali ya Marekani barani Afrika.
Symbion nchini inajenga mradi wa megawati 600 na pia itajenga njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 650.
Ina vituo vitatu vya kuzalisha megawati 217 za umeme Arusha, Dodoma na Dar es Salaam. Cha Ubungo kinazalisha megawati 112 kwa kutumia gesi.
MICHELLE ASISITIZA ELIMU
Mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama, ametaka kuepukwa mila na tamaduni zinazomkandamiza mtoto wa kike, ikiwemo kumkosesha haki ya kupata elimu, anaripoti Suleiman Jongo.
Michelle alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa wake wa marais wa Afrika.
Alisema endapo mila potofu dhidi ya mwanamke zitaachwa, harakati za mapambano dhidi ya umasikini zitafanikiwa. Miongoni mwa mila hizo alisema ni mfumo dume, ambapo kipaumbele cha elimu hutolewa kwa watoto wa kiume pekee.
Michelle alisema alizaliwa katika familia yenye kipato cha wastani na si tajiri, lakini wazazi wake hawakuwa na ubaguzi katika kuwasomesha, hivyo yeye na kaka zake walipata elimu sawa na kuwa kichocheo katika mafanikio yake.
Kwa mujibu wa Michelle, elimu kwa mtoto wa kike ni nyenzo muhimu itakayomrahisisha kutimiza majukumu ya nyumbani na katika jamii kwa jumla.
Alimpongeza Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete kwa jitihada za kuwasomesha watoto wa kike nchini.
Alisema amevutiwa na Mama Salma, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), kwa kuwasomesha watoto wa kike.
Rais Jakaya Kikwete akifungua mkutano huo, alisema mfumo dume bado unaendelea kutumika katika jamii mbalimbali barani Afrika, hivyo mabadiliko yanahitajika.
Alisema familia nyingi zinamtazama mwanamke kama mtu wa kukaa nyumbani, hastahili kupewa fursa muhimu, ikiwemo kumiliki ardhi na rasilimali nyingine za msingi.
Mama Salma kwa upande wake aliishukuru Taasisi ya Kuwawezesha Wanawake Duniani ya George W. Bush, ambayo ndiyo imedhamini mkutano huo kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji.
Alisema Tanzania inajitahidi kutekeleza majukumu ya msingi, ikiwemo kumuelimisha mwanamke na kukabiliana na maradhi, yakiwemo magonjwa ya ukimwi na malaria.
Kwa upande wake, Laura Bush, mke wa Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush, alisema mwanamke akielimishwa anakuwa msaada mkubwa katika jamii na taifa kwa jumla.
Aliwashukuru wake wa marais wa Afrika kutokana na hatua ya kushiriki mkutano huo. Alisema yeye na mumewe wanaunga mkono jitihada za ukombozi wa mwanamke duniani.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, Tony Blair, Cherie Blair. Pia wake wa marais wa Uganda, Msumbiji na Afrika Kusini.
FBI YAPONGEZA ULINZI
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), limepongeza timu ya ulinzi nchini, ikisema iko imara kiutendaji, anaripoti Rabia Bakari.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema hayo jana, baada ya Rais Obama na ujumbe wake kuondoka nchini.
Kova alisema maeneo ambayo yamepongezwa ni kumudu ratiba za kiusalama na operesheni ya ulinzi kwa jumla.
“Wenyewe wamekubali, wamesema wamekutana na watu wenye upeo katika ulinzi. Pia ushirikiano wa dhati waliopata wakati wote walipokuwa nchini kabla na baada ya rais wao kuja,” alisema.
Alisema mambo yote yalikwenda vizuri, kwani hakuna taarifa ya tukio lolote baya.
Hata hivyo, alisema wanakutana ili kutathmini ziara ya rais huyo na baadaye matokeo yatawekwa wazi kwa wananchi.
UMATI BARABARANI
Kabla ya Rais Obama kuondoka, shughuli za kijamii na kiuchumi zilisimama kwa muda kwenye baadhi ya maeneo ya jiji, anaripoti Mohammed Issa.
Umati ulijipanga kwenye barabara za Bagamoyo, Sam Nujoma, Morogoro, Mandela na Nyerere, ambako msafara wa Rais Obama na ujumbe wake ulipita.
Barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma zilifungwa kwa muda ili kupisha msafara wa rais huyo.
Katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo, baadhi ya wananchi walipanda juu ya ghorofa ili wamuone kiongozi huyo.
Baadhi ya waendesha bodaboda walipanda juu ya vyombo hivyo vya usafiri ili wamuone Rais Obama, aliyekuwa anakwenda kwenye mitambo ya kuzalisha umeme ya Symbion.
Katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo, abiria waliokuwa wasafiri mchana waliungana na wananchi wengine waliokuwa na shauku ya kumuona Rais Obama.
Ulinzi uliimarishwa mara dufu eneo hilo, ambapo kulikuwa na magari ya maji ya kuwasha, polisi wa kikosi cha mbwa na farasi, askari wa doria, upelelezi na askari wa SUMA JKT.
Maofisa usalama wa Marekani nao walitanda kila kona wakiwa na vifaa maalumu vya ulinzi.
Rais Kikwete aliwasili TANESCO saa 4.32 asubuhi, ambapo wananchi waliojipanga barabarani walimshangilia, ambapo baadaye helikopta ya polisi ilionekana ikifanya doria.
Saa 4.41 asubuhi, msafara wa Rais Obama ukiwa na magari 31 uliwasili Ubungo na kuibua shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.
Msafara huo uliondoka Ubungo saa 5.24 asubuhi kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya safari ya kurejea Marekani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru