Friday 5 July 2013

CCM Dar wampa ‘tano’ Kikwete


NA MOHAMMED ISSA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, kimesema Rais Jakaya Kikwete anastahili pongezi kutokana na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Kimesema tangu kuingia madarakani Rais Kikwete, uhusiano wa Tanzania na mataifa makubwa duniani unazidi kuimarika.
Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema juhudi zinazofanywa na Rais Kikwete katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa, zinastahili kupongezwa kwani mafanikio yanaonekana.
Madabida, alisema ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama na Rais wa China, ni juhudi binafsi zilizofanywa na Rais Kikwete na serikali yake.
Alisema ziara hizo mbali ya kuipatia heshima nchi, pia zimezaa matunda ya mafanikio kwa Watanzania.
Madabida alisema ujio wa viongozi hao, ni ishara tosha kuwa Tanzania ni kivutio kikubwa cha uwekezaji wa nje.
Kwa mujibu wa Madabida, Chama kinaendelea kuisimamia serikali katika kutekeleza ahadi zake ambazo kwa asilimia kubwa zimetekelezwa.
Alisema ujenzi wa barabara za lami unaoendelea mkoani humo, ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na juhudi za Rais Kikwete.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru