Monday, 8 July 2013

Membe kuongoza kikao cha SADC


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, atakuwa
Mwenyekiti wa kikao cha 15 cha Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Kikao hicho kinachohusisha sekta ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kitatanguliwa na
kikao cha Makatibu Wakuu na Maofisa Waandamizi, Julai 10 na 11, mwaka huu.
Kitahudhuriwa na nchi zote wanachama wa SADC, isipokuwa Madagascar, ambayo imesimamishwa uanachama.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilisema, pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitajadili hali
ya kisiasa kusini mwa Afrika na uimarishaji wa demokrasia.
Mengine ni pamoja na utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, mikataba ya ushirikiano katika nyanja za ulinzi na usalama, pamoja na ushirikiano baina ya SADC na Umoja wa Ulaya (EU).
Iliongeza kuwa, washiriki wa vikao vya maofisa waandamizi wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo, wakati Mawaziri watawasili Julai 12, mwaka huu.
Ilisema, kikao cha mawaziri kitakachofanyika Julai 13, kitafuatiwa na mkutano wa Wakuu wa Nchi, utakaofanyika Lilongwe, Malawi, Agosti 17 na 18, mwaka huu.
Mkutano huo utahitimisha Uenyekiti wa Tanzania wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, ulioanza Agosti, 2012.  Mwenyekiti anayefuata wa Asasi hiyo atakuwa Namibia, wakati Uwenyekiti wa SADC utachukuliwa na Malawi.
Nchi Wanachama wa SADC ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Sheli Sheli, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru