Sunday, 7 July 2013

Kataeni yanayovunja Muungano -Dk. Bilal


NA MOHAMMED ISSA
MLEZI wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka wananchi kuyakataa mambo yatakayovunja Muungano wakati wa kujadili Rasimu ya Katiba mpya.
Amesema jambo la msingi wakati wa kuipitia rasimu hiyo ni kuhakikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unalindwa na hauvunjiki.
Dk. Bilal, ambaye ni Makamu wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, amesema mchakato wa kupata katiba mpya usiibue vitu vipya, ambavyo vinaweza kulisambaratisha taifa.

Alisema hayo juzi, katika ukumbi wa Karimjee, mjini Dar es Salaam, alipofungua kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo.
Dk. Bilal alisema Muungano una faida kubwa na umewafanya Watanzania kuwa wamoja, hivyo kama kutakuwa na mambo yatakayouvunja ni vyema wananchi wakayakataa.
“Wakati wa kuipitia rasimu ya katiba mpya jambo la msingi na muhimu ni kuhakikisha tunaulinda Muungano.
“Muungano tulionao umetupa heshima kubwa kwenye anga za kimataifa, hivyo ni vyema tukaendelea kuudumisha na kuuenzi,” alisema.
Alisema wakati wa kuipitia rasimu ya katiba mpya ni vyema jamii ikahakikisha inalinda sifa njema zilizopo katika taifa.
Makamu wa rais alisema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha katiba ijayo inajenga nchi, inadumisha mema yaliyopo na iweke wazi rasilimali za taifa ili kila mtu aweze kufaidika nazo.
“Katiba isibomoe, isifarakanishe, isitugawe na isitutenge, tuijadili kwa kina na tuhakikishe inajenga umoja na mshikamano uliopo.
“Kama tunaendelea kuishi vizuri, nchi moja basi katiba isitugombanishe wala isitutofautishe,” alisema.
Dk. Bilal aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuipitia na kuchangia maoni katika rasimu ya katiba kwa umakini na kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alisema mkoa unampongeza Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumteua Dk. Bilal kuwa mlezi wa mkoa huo.
Alisema Dk. Bilal ni kiongozi makini na watampa ushirikiano wa hali na mali katika kukijenga Chaman

1 comments: