Wednesday, 3 July 2013

Nyalandu: Simba hatarini kutoweka


NA RABIA BAKARI
UJANGILI wa wanyama katika hifadhi za taifa nchini, umeendelea kushika kasi na sasa, majangili yamekuja na mbinu mpya ya kuwaua Simba.
Awali, ujangili huo ulijikita zaidi katika kuua Tembo kwa ajili ya meno, lakini sasa Simba nao wapo hatarini kufuatia moyo wake kudaiwa kutumika kwa imani za kishirikina.
Kufuatia hali hiyo, serikali inafanya mazungumzo na Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (Interpool) kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya tembo, simba na wanyama wengine.
“Tumetangaza rasmi kuwa ujangili ni janga la kitaifa, majangili sasa wameanza kuwaua mpaka samba.
“Na unazidi kushika kasi ukihusisha imani za kishirikina,” alisema Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Nyalandu aliyasema hayo jana, alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, katika viwanja vya Maonyesho ya 37 ya Kimataifa ya Biashara, Dar es Salaam.
Alisema lengo la kuzungumza na Interpool ni kutaka msaada wa kudhibiti njia zote zinazoingia katika nchi za Maziwa Makuu ikiwemo viwanja vya ndege na njia nyingine zinazotumika kupitisha nyara hizo.
Pia, alisema Serikali ya Marekani imekubali kusaidia jitihada za serikali katika kupambana na ujangili nchini.
“Wengi hasa katika nchi za Asia, wanaamini kuvaa bidhaa iliyotengenezwa na pembe za ndovu ama meno ya tembo kunaleta bahati.
“Na kama mwanamke hajaolewa, basi ataolewa na mtu tajiri..lakini sasa ujangili wa Simba umeshika kasi, wengi wanaamini mwanaume akipata moyo wake basi atakuwa na uwezo wa kuoa mwanamke zaidi ya mmoja, na imani nyinginezo,” alifafanua.
Hata hivyo, alisema serikali itawashughulikia wale wote wanaowatuma vijana kufanya vitendo vya ujangili na kuiba nyara za serikali bila kujali cheo wala itikadi.
“Vijana tunaowakamata kwa asilimia kubwa sio wahusika, hukamatwa wakiwa hawana hata viatu, wahusika ni wenye tai walioko huku mijini..hata wale watakaobainika kuwahifadhi watakuwa hatiani,” alisema Nyalandu.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa kuwafichua majangili na wafadhili wao ili kufanikisha ulinzi wa maliasili za nchi.
Nyalandu, alisema soko la utalii limepanda kwa kiasi kikubwa, na kwa mwaka jana, nchi iliingiza dola za kimarekani bilioni 1.5 (Sh.bilioni 24) na kusaidia pato la uchumi kwa asilimia 17.
Lakini kutokana na matukio ya ujangili, huenda kukaathiri maendeleo hayo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru