Tuesday 16 July 2013

Dk. Magufuli amshitukia mkandarasi


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli, amemshukia mkandarasi wa kivuko kinachotengenezwa mjini Dar es Salaam, na kuagiza Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), kumchunguza kama ana uwezo kutekeleza mradi huo.
Mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya Scheepsbouw Noord Nederland b.v ya Uholanzi, alipewa kazi kwa mkataba wa sh. bilioni 2,840, na kilitakiwa kukamilika tangu Februari, mwaka jana.
Dk. Magufuli alitoa agizo hilo jana alipotembelea kukagua maendeleo ya kivuko hicho eneo la bandari Dockyard, Kurasini mjini Dar es Salaam, na kuagiza kazi hiyo ikamilishwe kabla ya Agosti 30, mwaka huu.
Alisema utekelezaji wa kazi hiyo hauridhishi na kwamba, kivuko hicho kinatakiwa kutumika katika eneo la Msanga Mkuu kwa ajili ya kuhudumia wananchi kati ya eneo la Msanga Mkuu na Msemo, mkoani Mtwara.
“Mkandarasi huyo achunguzwe endapo kweli anao uwezo wa kutekeleza mradi huu na kama ana usajili halali wa kufanyakazi zake hapa nchini,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema mkandarasi huyo alipewa kazi ya ununuzi wa kivuko kipya tangu Juni 17, 2010, kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Msangamkuu mkoani Mtwara.
Dk. Magufuli, alisema kivuko hicho ni cha tani 50, ambacho kitabeba magari sita na abiria 100 kwa wakati mmoja.
Mkandarasi huyo alianza kazi rasmi Desemba, 2011, na alitakiwa kuikamilisha miezi 10 na kukabidhi rasmi Februari, 2012.
Hata hivyo, alisema muda ulipofika alishindwa kukabidhi kazi na kutakiwa aikamilishe Mei, mwaka jana.
Baadaye aliomba aongezewe muda hadi Desemba, mwaka jana, hata hivyo, alishindwa kuikamilisha kazi hiyo mpaka sasa.
“Mkandarasi huyo amekaa hapa karibu miaka mitatu na ameshalipwa asilimia 78 ya fedha za kazi, sioni sababu ya kuchelewa hivi, hata mafundi gereji wangekuwa wameshaikamilisha,” alisema Magufuli.
Waziri Dk. Magufuli, aliwatahadharisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuwa makini wakati wanapoingia mikataba ya aina hiyo.
Fedha hizo alizolipwa ni kwa ajili ya kuagiza kivuko na kinachoendelea sasa ni kukiunganisha ili kipelekwe Mtwara.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru