Wednesday 3 July 2013

Mtandao mabomu Arusha wabainika


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
MTANDAO wa ulipuaji mabomu katika Jiji la Arusha umebainika na kwamba, mipango yote ilianzia jijini humo, pamoja na wahusika wake.
Taarifa za awali kutoka Jeshi la Polisi zinasema milipuko iliyotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti na ule wa Uwanja wa Soweto inafanana, licha ya mabomu hayo kutengenezwa nchi tofauti.
Bomu lililolipuliwa uwanja wa Soweto, Juni 15, mwaka huu, limetengenezwa nchini China na lile la kanisani lililolipuliwa Mei 5, mwaka huu, imebainika lilitengenezwa Russia na halikuwa na namba ya usajili.
Imeelezwa wataalamu wa mabomu kutoka China wapo jijini Arusha wakifanya uchunguzi wa kina kuhusu bomu hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, amesema uchunguzi wa milipuko hiyo unaendelea na hakuna atakayebainika atakayeachwa atambe.
Mulongo alisema hayo jana, kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Alisema makachero wa polisi na  vyombo vingine vya ulinzi bado wapo jijini hapa wakiendelea na kazi na kwamba, mtandao wa walipuaji umebainika.
“Uchunguzi unaendelea, wa awali umebaini mtandao wa walipuaji mabomu. Matukio na mipango yote ilianzia hapa na muda si mrefu mbichi na mbivu zitawekwa hadharani,” alisema.
Alisema serikali itachukua hatua kali na zinazostahili kwa yeyote atakayebainika kuhusika na mtandao huo bila kujali cheo, kwani matukio hayo yameharibu sifa ya taifa kimataifa.
Mkuu wa mkoa alisema idadi kubwa ya wananchi ilijitokeza kutoa ushahidi wa watu waliohusika katika matukio hayo na kwamba, kazi hiyo inafanyika kwa umakini ili kuepuka kukamatwa wasiohusika.
“Wananchi ni watulivu na wanashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, hatutaki kufanya makosa kwenye kazi hii,” alisema.
Mulongo aliwaonya wanasiasa na kuwaasa kuacha kutumia milipuko hiyo kama ajenda za kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kuongeza maumivu kwa walioathirika na kupoteza ndugu zao.
“Wanasiasa wamekuwa wakitumia uongo mwingi dhidi ya serikali na kuichafua nchi duniani, hivi tunajiuliza ni kwa faida ya nani?
“Ni wakati sasa wa kuacha dharau ya wazi kwa vyombo vya dola, kama huviheshimu ni mwanzo wa kuvuruga amani mbele ya safari,” alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru