- Acharuka kwa kucheleweshwa kwa ahadi yake
- Atoa siku saba, wananchi wapagawa kwa furaha
Na mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kilosa, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga wa mafuriko.
Mafuriko hayo yalitokea miaka minne iliyopita mjini Kilosa,
ambapo Rais Kikwete aliagiza wahanga kupewa viwanja.
Alitoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa Kilosa
katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea wilaya
hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na
wahanga hao kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya
kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea
kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa.
“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,” alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao kuhusu ahadi hizo.
Baada ya kuambiwa kuwa vimepimwa viwanja 800 katika halmashauri
hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao
wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho (jana) hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote ziwe zimekamilika na kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazungumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete.
Mapema, Rais Kikwete
ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la Msolwa,
Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda
Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo
lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini Hydropower Project unajengwa kwenye milima na maporomoko
ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na 2.3 kwa ajili ya
mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule maarufu na ya mfano
ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka
1994.
Mradi huo ambao unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama
kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa
na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na
Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja
kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao utaanza kuzalishwa Januari
mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Umeme Vijiji–
REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa
Morogoro leo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru