Thursday, 14 August 2014

Mbwa wenye kichaa waua mwanafunzi  •  Wananchi wenye hasira wawaua na kuwachoma moto

Na Mwandishi Wetu
MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi Ludewa mkoani Njombe, Iblahim Chipungahelom ameuawa na kisha kuliwa nyama na mbwa wanaodaiwa kuugua kicha kwa kukosa chakula kwa muda mrefu.
Tukio hilo la kusikitisha na lililoleta simanzi kubwa kwa wakazi wa Ludewa Mjini, lilitokea Agosti 8, mwaka huu, saa saba mchana katika eneo la Ikulu, ambapo mtoto huyo na wenzake walikuwa wakipita jirani na nyumba ya Bosco Lingalangala kwenda kuchuma mapera.
Mashuhuda wa tukio hilo, Mama Kumba na Mama Haule, wakazi wa kitongoji cha Ibani katika kata ya Ludewa, walisema wakiwa nyumba, walisikia kelele za watoto jirani huku wakimwita mwenzao, ambaye sasa ni marehemu bila mafanikio.
“Tulipowauliza walisema kuwa mwenzao, Ibrahim amekamatwa na mbwa na ndipo tulipokusanyika na kwenda kumwokoa, lakini tulipofika eneo la tukio, tulimkuta mbwa wakiendelea kumla huku akiwa amelala kifudifudi, lakini tulishindwa kumwokoa na kutoa taarifa polisi,î walisema akina mama hao kwa uchungu.
Mganga wa Hospitali ya Ludewa, Sira Rajabu, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa mtoto Ibrahim, alisema ulikuwa na majeraha makubwa mwili mzima huku paja la mguu wake wa kulia likiwa limeliwa na kuondolewa nyama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgensi Ngonyani, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa upelelezi unaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali, akiwemo mmiliki wa mbwa hao ambaye inasadikika kuwa anaishi jijini Dar es Salaam.
Mganga wa Mifugo, Simoni Haule, alisema mbwa hao ni wa Lingalangala, hawajapata chanjo zaidi ya miaka miwili sasa kwa hiyo tayari wanaugua ugonjwa wa kichaa, ambacho hawawezi kupona tena na dawa iliyobaki ni kuuawa.
Mmiliki wa mbwa hao, Lingalangala hakupatikana ili kuzungumzia suala hilo kwa sababu simu yake ya mkononi haikupatikana.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Ludewa, Monica Mchiro, aliwatahadharisha waombolezaji na wananchi waliohudhuria mazishi kuwa, mawasiliano yamefanywa kati yake na mmiliki wa mbwa hao, lakini majibu aliyoyatoa hayana ushirikiano kwa sababu ameahidi kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote
atakayehusika kuwadhuru mbwa wake.
Maelezo hayo yaliamsha hasira za wakazi na kuamua kuanzisha msako mkali dhidi ya mbwa hao, ambapo waliwatia mikononi na kuwaua wote kisha kuwachoma moto hadharani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru