Tuesday, 26 August 2014

Nape awarushia kombora UKAWANA MWANDISHI WETU
MCHAKATO wa Katiba Mpya umeendelea kutumika kama kichaka cha kuzuia vuguvugu la mabadiliko katika vyama vya upinzani nchini.
Vyama vingi vya upinzani vikiwemo vinavyojinadi kuwa ndio vikubwa, vimekuwa kwenye migogoro mikubwa inayotokana na ubaguzi, matumizi mabaya ya madaraka na kugombea ruzuku.
Pia vyama vingine ikiwemo CHADEMA ambacho kimegubikwa na migogoro mizito ikiwemo ya kuwania madaraka na ufujaji wa fedha za ruzuku, huku baadhi ya viongozi wake wakitimuliwa na wengine kuamua kujiengua wenyewe.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana kuwa vyama hivyo katika kufunika hoja hiyo, wamebuni njia mbalimbali ikiwemo kuunda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema viongozi wa vyama hivyo vilivyounda UKAWA, wamekuwa kwenye wakati mgumu mbele ya wanachama wanaopenda mabadiliko na kwamba, mchakato wa Katiba Mpya ndio umetumika kupunguza makali.
Akizungumza ofisini kwake mjini Dar es Salaam, Nape alisema viongozi wa vyama hivyo hawataweza kuepuka vuguvugu hilo kwa kujaribu kukwepesha hoja na kujificha nyuma ya UKAWA.

“Katiba mpya haiwezi kupatikana kwa maandamano. Maridhiano hayawezi kupatikana kwa maandamano. CCM hatuna tatizo na mikakati hiyo, lakini wasifiche migogoro yao kwa mgongo wa Katiba,” alisema.

Nape alisema CCM inaaamini kwamba Katiba mpya itapatikana kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kukaa bungeni kujadiliana na hatimaye kufikia muafaka.
Alisema yapo mazungumzo yanayoendelea, lakini anashangazwa na kauli kung’ang’ania kwamba watafanya maandamano nchi nzima kupinga mchakato huo.
Kwa mujibu wa Nape mambo yanayoendelea kujadiliwa ndani ya Bunge hilo ni muhimu na yana maslahi makubwa kwa Watanzania hivyo UKAWA kuendelea kususia ni kuwasaliti waliowachagua.
Hivi karibuni kumekuwa na migogoro ndani ya CHADEMA iliyosababisha baadhi ya wanachama wake kukihama na kuanzisha chama kipya cha ADC na kwamba, bado kimeendelea kukumbwa na migogoro inayosababishwa na uchaguzi unaendelea ndani ya chama hicho.
Hatua hiyo ilisababishwa na baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho kukiendesha kwa ubabe kwa kuwatimua baadhi ya wanachama waliokuwa wakiwapinga katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa CHADEMA.
Katika hali ya kushangaza, pia aliyekuwa mwanachama wa chama hicho Habibu Mchange, aliibuka na kuweka hadharani mambo mazito yanayofanywa na CHADEMA.
Mchange, ambaye alizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam na pia kupitia vituo vya redio na televisheni, alieleza namna matukio ya mauaji na utekaji yanavyopangwa na kutekelezwa ndani ya chama hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru