Thursday, 14 August 2014

Shahidi aeleza trafiki feki alivyopata sare za polisi


NA SYLVIA SEBASTIAN
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, imeelezwa kuwa mshitakiwa James Hassan (45), anayedaiwa kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, alijipatia kofia na mkanda baada ya kufa kwa baba yake mdogo na kisha kushona sare za kikosi hicho.
Koplo Julius (36), ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa  Jamhuri, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, alipokuwa akitoa ushahidi.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Felista Mosha, Koplo Julius alidai Agosti 14, mwaka jana, akiwa katika Kituo cha Polisi cha  Stakishari, alifika mtuhumiwa akiongozana na Inspekta Peter.
Koplo Julius alidai mtuhumiwa huyo alikuwa amevalia sare za  trafiki mwenye cheo cha Sajini. Alidai alipewa jukumu la kuchukua maelezo yake na kabla hajaanza kuyachukua, alimpa haki zake za msingi za kuwa na ndugu au wakili.
Alidai mshitakiwa alimweleza yuko tayari kutoa maelezo peke  yake.
Shahidi huyo alidai katika maelezo yake, mshitakiwa huyo  alimweleza kwamba katika familia wamezaliwa watatu na  wawili walishafariki na alisoma shule ya msingi Tarime, wakati  huo akiwa anaishi na baba yake mdogo.
Alidai mwaka 1991, mshitakiwa alijiunga na Chuo cha Polisi cha CCP Moshi na hakuweza kumaliza kozi yake kwa kuwa alifukuzwa baada ya kuitishwa ‘lokoo’.
Koplo alidai baada ya kufukuzwa, mshitakiwa alirudi nyumbani  kwa baba yake mdogo, ambaye alikuwa
askari wa Kikosi cha  Usalama Barabarani mwenye cheo cha Sajini, ambaye  alifariki mwaka 2012.
Shahidi alidai mshitakiwa baada ya baba yake mdogo kufariki, alijipatia mkanda na kofia na kwenda mkoani Tabora, ambako alishona nguo za trafiki, zikiwa na cheo cha sajini.
Alidai mshitakiwa alipofika Dar es Salaam, alianza kuongoza  magari  katika maeneo ya Kinyerezi na alikamatwa maeneo hayo. Kesi  hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Agosti 27, mwaka huu.
Mshitakiwa huyo anadaiwa Agosti 14, mwaka jana, alikamatwa  akiwa na sare za kikosi hicho, akijifanya mtumishi wa umma.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru