Thursday, 14 August 2014

Hatutaingia vitani na Tanzania- Mutharika  •  Asisitiza Ziwa Nyasa lote la Malawi tangu 1910

LILONGWE, Malawi
RAIS Peter Mutharika, amekanusha uwezekano wa Malawi kuingia vitani na Tanzania kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili kwenye Ziwa Nyasa, lakini amesema suala hilo halina mjadala tena.
Mutharika alitoa msimamo huo juzi mjini hapa baada ya kuwasili kutoka Washington, DC Marekani, alikohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na Marekani.
“Ndiyo, nilisema Ziwa halina mjadala, ila sikusema tutakwenda vitani na Tanzania,” alisema Mutharika akikaririwa juzi na vyombo vya habari mjini hapa alipokuwa akizungumza na wanahabari.
Kiongozi huyo alijinasibu kuwa mtu wa amani, akisema: “Sipigani, isipokuwa mtu akinichokoza.”  Lakini akasisitiza kuwa, Ziwa lote la Nyasa ni mali ya Malawi.
“Hatutaingia vitani, lakini Ziwa hili limekuwa letu tangu miaka 104 iliyopita. Sheria iko wazi, nadhani kuna fursa ndogo sana ya kujadili hili, lakini naamini tutapata njia ya kulimaliza na Tanzania,” alisema.
Mutharika alisema alipokutana na Rais Jakaya Kikwete, Washington, DC, pamoja na mambo mengine, walijadili masuala ya uvuvi katika Ziwa hilo kwa wananchi wa pande zote mbili. 
Alisema serikali yake itapitia taarifa aliyowasilisha mtangulizi wake, Joyce Banda kwa viongozi wa zamani wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)na kuona nini cha kufanya.
“Tutaruhusu mchakato wa majadiliano kuendelea baina ya nchi hizi mbili na kuangalia yalifikia wapi,” alisema.
Mgogoro huo wa mpaka umekuwa ukiibuka na kufifia tangu Tanzania na Malawi zipate uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ulaya katika miaka ya mwanzo ya sitini.

Kamuzu Banda
Muasisi wa Taifa la Malawi, Hasting Kamuzu Banda, anaripotiwa kupata kumwonya mwenzake wa Tanzania, Rais Julius Nyerere  kuachana na Ziwa hilo au akaribishe hatari ya mgogoro wa kivita.
Lakini suala hilo liliibuka tena pale utawala wa kaka wa Rais wa sasa, Bingu wa Mutharika, alipoingia mkataba na Kampuni ya Surestream ya Uingereza, kufanya uchunguzi wa kuona kama upo uwezekano wa kupatikana akiba ya mafuta katika eneo la Kaskazini mwa Ziwa hilo.
Tanzania ilionya wakati huo, kwamba itadungua ndege yoyote ya uchunguzi itakayoruka katika anga lake ziwani humo. 
Lakini Malawi bado inatetea madai yake kuwa Ziwa hilo lote ni lake kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland wa Julai 1890, ambao uliandaliwa kati ya Uingereza na Ujerumani, ukibainisha maeneo ya makoloni hayo mawili na kuipa Ujerumani utawala wa Tanzania na Uingereza kuitawala Malawi, ikiwa ni pamoja na Ziwa lote.
Leo, kamati ya viongozi wa zamani wa SADC, wakiongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano, wanaendesha mazungumzo juu ya mgogoro huo. 
Mutharika (74), ambaye aliingia madarakani kwa uchaguzi wa Mei 20, mwaka huu, ambao hata hivyo ulibishaniwa, alisema alikutana na Rais Kikwete na alimwalika aje avue ziwani humo.
Wamalawi na Watanzania wanaoishi katika wilaya za mpakani mwa nchi hizo, wamekuwa wakifanya hivyo kwa amani huku wavuvi na wasafirishaji bidhaa wakiendelea kutumia Ziwa hilo bila matatizo hadi mgogoro huo ulipoibuka tena. 
Tangu kuibuka upya kwa mgogoro huo, uliochukua miongo kadhaa sasa, Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda alipata kudai kuwa Tanzania imejiimarisha kijeshi ziwani humo na kwamba wavuvi wa nchi yake wamekuwa wakinyanyaswa.
Banda - Rais wa pili mwanamke katika Afrika, naye alipata kukutana na Rais Kikwete kujadiliana juu ya Ziwa hilo katika mkutano wa SADC jijini Maputo, Msumbiji na jijini New York, Marekani kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa. 
Mwaliko wa JK
Wakati  Rais Mutharika akisema amemwalika Rais Kikwete akavue katika Ziwa Nyasa, Jumamosi iliyopita, vyombo vya habari vya Tanzania vilimkariri kiongozi huyo kupitia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Tanzania, akisema amemwalika kuitembelea nchi hiyo kwa ziara ya kiserikali na kutaka kumalizika kwa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya nchi hizo mbili.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kurugenzi hiyo, Rais Mutharika alimwalika Rais Kikwete kwa dhana ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili na kudumisha udugu.  
Taarifa ilisema wakati wa mazungumzo kati ya viongozi hao jijini Washington DC, Rais Mutharika alisema Tanzania ni nyumbani kwake kwani  alipata kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru