Wednesday, 27 August 2014

CCM yanena kuhusu Dk. Salim


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema taarifa zilizoripotiwa na gazeti la Dira ya Mtanzania kuhusu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama  Dk. Salim Ahmed Salim, hazina ukweli.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijinui Dar es Salaam jana, ilisema habari hiyo iliyochapishwa kwenye toleo la Jumatatu yenye kichwa cha  ‘CCM yamsulubu Dk. Salim mbele ya JK’, kuwa ni uzushi na imelenga kujenga chuki na uhasama.
Katika habari hiyo, gazeti hilo lilidai kuwa Dk. Salim amegeuzwa mbuzi wa kafara kwa kushambuliwa kwenye vikao vya Kamati Kuu ya CCM, kikiwemo kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
“CCM inasisitiza kuwa habari hiyo si ya kweli, imeandikwa kwa lengo la kugombanisha, kujenga chuki na uhasama baina ya Chama. Pia kumchafua kwa makusudi Dk. Salim,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dira ya Mtanzania ilidai kuwa Dk. Salim aliwekwa kitimoto akitakiwa atoe ufafanuzi ni kwa vipi Tume ya Marekebisho ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, ilikuja na mapendekezo ya serikali tatu huku takwimu zikionyesha waliotaka muundo huo ni wachache.
Katika taarifa yake hiyo, CCM ilisema katika vikao vyote vya Kamati Kuu, hakuna mwanachama au mjumbe yeyote ambaye amesakamwa kwa namna yoyote iwe kwa maneno au majibizano ya kawaida.
“Vikao vyote vya Kamati Kuu ya CCM, chini ya Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete, vimekuwa vikifanyika kwa amani na utulivu na hakuna mjumbe yeyote, ambaye amewahi kurushiwa maneno kwa namna yoyote ile,” ilisisitiza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru