Wednesday, 13 August 2014

Vigogo UKAWA sasa waweseka



  • Waibuka na masharti mapya kwa JK, Sitta
  • Wadai waliowasaliti wamesukumwa na njaa
  • Haki za wanaume zapigiwa upatu Katiba mpya
  • Mjumbe aliyepigwa, apiga kura akiwa kitandani

NA WAANDISHI WETU, DAR NA DODOMA
BAADA ya Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao vyake kwa utulivu, viongozi wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameibuka na kutoa masharti mapya.
Masharti ya kundi hilo ambalo limesusia vikao vya bunge hilo kutokana na kujali maslahi yao binafsi ikiwemo ya kusaka madaraka, ni ishara ya kuweweseka baada ya kuona dalili za kutoungwa mkono na wananchi.
Jana, viongozi hao walimtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha vikao vya bunge hilo vinginevyo watawaongoza wananchi kuingia barabarani kufanya maandamano.
Pia wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza kile walichodai ufisadi katika Bunge Maalumu la Katiba.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya CUF, James Mbatia (NCCR-MAGEUZI), Freeman Mbowe (CHADEMA) na Profesa Ibarahim Lipumba (CUF), walisema watashawishi wananchi nchini kote kuingia barabarani.
Kauli hiyo yenye lengo la kuzusha machafuko, inakuja wakati baadhi ya wajumbe wanaounda kundi hilo wakiamua kurejea bungeni kutokana na kubaini umoja huo hauna dhamira ya dhati na Watanzania.
“Iwapo Rais Kikwete atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha bunge hilo, tutawaongoza Watanzania kufanya maandamano kupinga,” alisema Mbatia ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR- Mageuzi.
Naye Mbowe alisema kitendo cha baadhi ya Wabunge wa chama kwenda Bungeni kuendelea na vikao alidai ni ‘wasaliti wa taifa’.
“Mtu kuingia bungeni si ‘issue’ vyombo vya habari viripoti habari za msingi na si njaa ya mtu mmoja mmoja,” alisema na kuongeza kuwa suala la Said Arfi (Mpanda Mjini-CHADEMA) na wenzake waliosaliti litashughulikiwa katika vikao vya chama.
Kuhusu Mbunge wa Maswa, John Shibuda kudai kuwa aliahidiwa kupewa helikopta alisema hana uhakika ahadi hiyo ilitoka wapi kwa sababu hana ufafanuzi wa kina wa suala hilo.
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alidai Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, ni mbadhirifu kwa sababu alipokuwa Spika wa Bunge, alijenga Ofisi ya Spika katika jimbo lake la uchaguzi la Urambo.
HAKI ZA WANAUME
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamependekeza suala la haki za wanaume kuingizwa kwenye Katiba kama ilivyo kwa makundi mengine.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tisa, Kidawa Hamid Salehe, alisema mapendekezo hayo yalijitokeza wakati wakijadili Sura ya Pili na ya Tatu ya Rasimu ya Katiba.
Alisema baadhi ya wanaume ambao ni wajumbe wa kamati hiyo walidai kuwa hivi sasa haki nyingi zimewekwa kwa wanawake tu.
Alisema haki hizo pamoja na kuwekewa mkazo katika sehemu nyingi bado wanaume wameachwa bila kuwa na haki zozote kikatiba, jambo ambalo sasa ni lazima lifike mwisho.
“Walilalamikia kuhusu suala la haki za wanaume na kudai kuwa kuna baadhi ya wanaume wamekuwa wakinyanyaswa na wake zao lakini wamekuwa kimya,’’ alisema.
Hata hivyo, alisema mbali na mvutano uliokuwepo, kamati hiyo imekubaliana kuliweka kando suala hilo na kulifikisha katika Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya majadaliano zaidi.
Akizungumzia Sura ya Tatu ambayo inahusika na maadili ya viongozi, Kidawa alisema wajumbe wamekubaliana kwa pamoja na wameweza kupata theluthi mbili kutoka kila upande baada ya kupiga kura.
Katika hatua nyingine, mjumbe aliyelazwa katika Hospitali ya Rufani  ya Mkoa wa Dodoma, Thomas Mgoli, baada ya kupigwa na wafuasi wa CHADEMA, jana alilazimika kupiga kura kupitisha baadhi ya sura za rasimu akiwa kitandani.
Mgoli, ambaye ni mjumbe wa Kamati Namba 12 katika kupiga kura kwake alitumia kura ya wazi lakini alipinga ibara ya 39 ya Sura ya Pili ambayo pamoja na mambo mengine inazungumzia masuala ya haki za binadamu.
Katika ibara hiyo, kuna kifungu kinachotoa ruhusa kwa wafungwa walemavu kuingia na magongo yao wakiwa kifungoni. jambo ambalo Thomas alilipinga.
Mgoli alisema hawezi kupitisha hilo kwani mfungwa anaweza kutumia magongo hayo kuwadhuru wengine akiwa gerezani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru