Thursday, 21 August 2014

Dk. Sheni ataka kuboreshwa uchunguzi wa afya


NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amezitaka nchi za  Mashariki, Kati na Kusini mwa Bara la Afrika kuimarisha huduma za maabara na utoaji wa elimu na uchunguzi wa maradhi ‘pathologia’.
Aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Mikutano wa Afrika Mashariki, mjini Arusha, wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Jumuiya ya APECSA kutoka Kanda ya Mashariki, Kati na Kusini mwa bara la Afrika.
Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, kwa  mwaka huu pia ulijumuisha wataalamu kutoka Uingereza. Maudhui  yake ni ‘umuhimu wa  huduma za maabara katika kutoa huduma bora za afya’.
Dk. Sheni, katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo,  alisema nchi wanachama wa jumuia hiyo zina jukumu la kuimarisha na kuendeleza huduma za uchunguzi wa maradhi na uimarishaji wa maabara.
Kutokana na uhaba wa wataalamu katika masuala ya uchunguzi na maabara sambamba na ongezeko la idadi ya watu,  alizitaka nchi hizo kutoa mafunzo katika fani hiyo pamoja na kuzingatia mazingira ili kuwavutia vijana waliowengi kujiunga na vyuo vinavyotoa taaluma hiyo.
Dk. Sheni alisema uhaba wa wataalamu hao uliopo isiwe kikwazo cha utoaji wa huduma bora za uchunguzi wa maradhi huku akiipongeza  APECSA  kwa kuanzisha chuo kwa ajili ya madaktari katika fani hiyo na kuonesha matumaini yake katika kuimarisha hadhi ya taaluma hiyo.
Alisema usomeshaji wa fani hiyo una gharama kubwa hivyo aliwataka wale wote wanaopata fusa ya mafunzo kuzingatia suala zima la uzalendo na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na utaalamu walionao katika utendaji wa kazi zao za utoaji wa huduma za afya kwa jamii.
Aidha, Dk. Sheni alisema licha ya huduma bora za kimaabara kuwa ghali,  aliwasihi wataalamu hao kutojali hilo na badala yake kuzingatia maisha ya jamii zaidi na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa huku akisisitiza haja kwa nchi husika kuzingatia bajeti katika masuala ya utoaji wa huduma hizo za uchunguzi na maabara.
Dk. Sheni alitoa wito kwa taasisi, idara na vitengo vyote vinavyohusika katika utoaji wa huduma hizo za uchunguzi kwa jamii kupatiwa fedha zinazohitajika kwa muda muwafaka ili viweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Katika hotuba yake hiyo, alieleza haja ya kuongeza wataalamu kwenye huduma hiyo  na kuwataka wana- APECSA  kufanya kazi na serikali za nchi zao  ili kuimarisha sekta ya afya na kueleza matumaini yake ya  mkutano huo  ambao hatimae mapendekezo yake yatasaidia kupambana na hali ya uhaba wa wataalamu wa fani hiyo.
Alitoa wito kwa washiriki kuangalia uwezekano wa kuiokoa hali iliyopo sasa katika utoaji wa huduma ya uchunguzi katika mwili wa binaadamu ili irudi kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Pia alizitaka serikali za nchi hizo husika kuekeza katika utoaji wa mafunzo pamoja na utoaji wa dhana zinazohitajika kwa madaktari hao.
Dk. Sheni, ambaye pia ni mtaalamu wa fani hiyo na mwasisi wa APECSA, alionyesha furaha yake ya kukutana na wataalamu wa aina hiyo na kutoa shukurani kwa washiriki wote wa mkutano pamoja na wote waliochangia kuufanikisha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru