Wednesday, 6 August 2014

Kikwete awapa somo Wamarekani


Na mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka sekta binafsi na wafanyabiashara wa Marekani kujifunza kutoka kwa wenzao wa Bara la Asia, ambao wameongeza uwekezaji barani Afrika.
Amesema hatua hiyo inatokana na kuwa wawekezaji hao wanapata taarifa sahihi na za ukweli kupitia vyombo mbalimbali.
Aidha, Rais Kikwete amesema pingamizi kubwa la kufanya biashara kati ya Marekani na Afrika sio tena Bahari ya Atlantic ama umbali, bali ni maono hasi yanayojengwa na vyombo vya habari vya Marekani kuhusu Bara la Afrika.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi wakati wa sherehe ya kuwekwa kwa Rais Kikwete katika Jumba la Mashujaa wa Uongozi wa Afrika la Jarida la African Leadership– African Leadership Hall of Fame – kwenye Jengo la National Press Club mjini Washington D.C., Marekani ambako Rais anafanya ziara ya siku tisa.
Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tatu wa Afrika kutunukiwa heshima hiyo kubwa. Marais waliotangulia kupewa heshima hiyo ni Rais wa Sierra Leone na Rais wa Namibia.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa medali na cheti cha kutunukiwa heshima hiyo, Rais Kikwete alisema ni jambo la kusikitisha kuwa vyombo vya habari havijali sana maendeleo mazuri ya Bara la Afrika. 
“Matokeo yake ni kwamba sekta binafsi ya Marekani imefanywa kuamini kuwa Bara la Afrika ni bara hatari sana kuwekeza,”alisema na kuongeza:
 “Mara nyingi Afrika inaonekana kama nchi moja badala ya Bara moja, na hivyo tatizo katika nchi moja kwa urahisi sana linafanywa tatizo la nchi zote na kwa namna hasi. Hii ni tofauti na Bara la Asia, ambako vyombo vya habari huelezea picha nzuri za matukio ya Afrika. Hii ndiyo maana kuna ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi ya Asia katika Afrika leo kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.”
Rais Kikwete ameongeza: “Hivyo, pingamizi kubwa la kufanya biashara kati ya Afrika na Marekani siyo Bahari ya Atlantic wala umbali kati ya maeneo hayo. Pingamizi ni maono hasi. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Rais Obama kwa uongozi wake na dhamira yake katika kubadilisha gurudumu hili la historia.”
 “Uamuzi wake wa kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na kuiwekea Sekta Binafsi ya Marekani ushiriki muhimu katika mkutano huu ni uamuzi wa kimapinduzi. Afrika imekuwa inasubiri fursa hii ya kufanya biashara na Marekani kwa muda mrefu. Na tumedhamiria kutumia fursa hii kwa kadri inavyowezekana,”alisisitiza.
Rais Kikwete amelishukuru Jarida la The African Leadership kwa mchango wake mkubwa wa kujenga uhusiano kati ya Afrika na Marekani.
Aidha, Rais Kikwete amelishukuru Jarida hilo kwa kumtunuku tuzo ya Kiongozi Bora wa Kusukuma Maendeleo Mwaka 2013 (The Most Impactful African Leader of the Year Award 2013), tuzo ambayo Rais Kikwete alipewa Aprili 9, 2014. Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru