Wednesday, 6 August 2014

Taaluma vyuo vikuu sasa kwa mtandao


NA WILLIAM SHECHAMBO
HATIMAYE serikali imezindua mradi wa ujenzi wa mtandao wa Internet kwa vyuo vya elimu ya juu na taasisi za utafiti nchini, ambao utaziunganisha na kuziwezesha kushirikiana katika masuala ya kitaaluma.
Mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, mara utakapokamilika, unatarajiwa kuziunganisha taasisi 28 huku zingine zikipewa fursa ya kujiunga na mradi huo kwa kadri inavyowezekana.
Serikali ya awamu ya nne imekuwa ikiweka mkazo mkubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA).
Katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam jana kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo ni mafanikio makubwa kitaaluma.
Hata hivyo, alisema mradi huo ambao ulianza ujenzi wake mwaka 2008, umechelewa kukamilika hivyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi Watanzania.
Alisema zipo sababu kadhaa zilizosababisha hali hiyo, ikiwemo matatizo ya makandarasi, ambao walisababisha kuwepo ufinyu wa fedha, ambazo kadri muda unavyosogea, ndivyo thamani yake inabadilika.
“Fedha (Dola) tulizopewa na WB zinabadilika thamani kadri muda unavyokwenda, mkandarasi alikuwa hajakamilisha ujenzi wa mtandao, hivyo alitafutwa mwingine ambaye mpaka anaanza kazi, muda ulishapotea,” alifafanua.
Mbarawa alisema hatua hiyo ilisababisha Benki ya Dunia kutaka kujitoa kwenye mradi huo, hali iliyomlazimu kuwasiliana na wakuu wa vyuo kadhaa ili kutoa msaada kifedha kwa ajili ya kupatiwa huduma ya mtandao kupitia mkongo wa taifa.
Hata hivyo, alisema utaratibu huo uliofanikiwa mpaka sasa, unadhihirisha nia ya serikali ya kuwekeza kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA), kupitia mkongo wa taifa wenye huduma bora na nafuu, ambapo elimu ya juu nchini itapata fursa za kushirikiana kwa rasilimali zilizopo kwenye taasisi husika na jirani.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa matumizi ya TEKNOHAMA nchini yanakuwa kama yalivyokusudiwa kwa kupambana na usalama wa matumizi katika mtandao, Waziri Mbarawa alisema wizara yake imeandaa sera tatu 
zitakazosimamia utumiaji sahihi wa mtandao, ambazo zitawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa huku pia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikifanya kila jitihada kulisimamia hilo.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Kaboko Kahiga, alisema Watanzania wanatakiwa kutumia vizuri teknolojia hiyo katika malengo yaliyokusudiwa na kwamba taasisi zote za elimu zihakikishe zinajiunga  ili kuliletea maendeleo taifa kupitia teknolojia hiyo, ambayo itawapa soko kimataifa kutokana na maendeleo ya utandawazi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru