Thursday, 7 August 2014

Kiongozi wa Uamsho kizimbani  •  Ahoji kushitakiwa Bara badala ya Z’bar

NA MWANDISHI WETU
KIONGOZI wa Jumuia ya Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, anayetuhumiwa kuhifadhi wahusika wa ugaidi, amesomewa mashitaka upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Wakati hatua hiyo ya kisheria ikichuliwa dhidi yake, Sheikh Farid alihoji mahakamani hapo juu ya uhalali wa yeye na wenzake 20 kufikishwa katika mahakama ya Bara, wakati wamekamatwa Zanzibar, ambako ni nchi kamili.
“Tunashangaa kushitakiwa hapa, labda Zanzibar sio nchi, wakati kuna Mahakama Kuu, Mwanasheria Mkuu, Jaji na vitu vingine.
“Sote tumekamatwa Zanzibar, tunashangaa kuletwa hapa, tumeletwa Tanganyika kuonewa. Zanzibar ni nchi, kuna mwanasheria mkuu, mahakama kuu, jaji, tumeletwa huku kama Zanzibar sio nchi,” alilalamika Sheikh Farid.
Mshitakiwa huyo alitoa malalamiko hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, muda mfupi kuunganishwa na washitakiwa wenzake na kusomewa mashitaka upya.
Sheikh Farid alisomewa mashitaka upya baada yeye na Jamal Noordin Swalehe, kufutiwa mashitaka yaliyokuwa yanawakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Warialwande Lema.
Mbali na Farid na Jamal, washitakiwa wengine ni Nassoro Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassani au Jibaba, Hussein Ally, Juma Sadala na Said Ally, Hamis Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange au Mapala na Amir Juma na Kassim Nassoro na Salehe Juma.
Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Peter Njike, akishirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, na Wakili wa Serikali George Barasa, uliomba kufanya mabadiliko ya hati ya awali ya mashitaka iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa 16 kwa kuwaongeza Farid, Jamal, Kassim na Said.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka manne ya kula njama za kutenda kosa, kuingiza watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda vitendo vya kigaidi, kutafuta watu kushiriki kufanya vitendo hivyo na kuhifadhi watu waliotenda vitendo hivyo.
Akiwasomea mashitaka Barasa alidai tarehe tofauti kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014 katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washitakiwa wote walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kutafuta watu wa kushiriki vitendo vya kigaidi.
Katika shitaka la pili, washitakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho huku wakijua walikubaliana kuwaingiza kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki vitendo vya ugaidi.
Sheikh Farid anadaiwa katika kipindi hicho huku akijua aliwaingiza nchini Sadick na Farah ili kushiriki katika vitendo vya kigaidi na kwamba aliwahifadhi watu hao, huku akijua wametenda vitendo hivyo.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Kabla ya  kuahirishwa kwa kesi hiyo, washitakiwa hao walilalamikia kitendo cha kunyimwa kusalimiana na ndugu na jamaa zao wawapo mahabusu gerezani.
Sheikh Farid alidai wengi wao kwa hapa hawana ndugu wa karibu kama vile mke, baba na watoto, hivyo wanaomba jamaa zao wanaokuja kuwasalimia kuruhusiwa.
Hata hivyo, Wakili Njike alidai hadhani kama kuna maelekezo ya namna hiyo ya kuwazuia washitakiwa wasionane na ndugu zao.
Hakimu Hellen alisema kutokana na upande wa Jamhuri kueleza hayo, lakini lazima kuwe na kiwango cha watu wanaozungumza nao.
Washitakiwa hao walirudishwa rumande hadi Agosti 21, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Sheikh Farid na wenzake waliondolewa mahakamani hapo kwenda mahabusu kwa kutumia basi kubwa la Magereza, huku likiwa na msafara wa magari matatu ya polisi na Magereza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru