Thursday, 14 August 2014

Dk. Kamani apewa tunzo ya utendaji bora Afrika


Na Mwandishi Wetu
NYOTA ya Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani, imeendelea kung’ara kutokana na kuonyesha utendaji bora katika kusimamia sekta ya mifugo nchini.
Kwa hali hiyo, Dk. Kamani, ambaye pia ni mbunge wa Busega, amepewa Tunzo ya Utawala Bora katika kipengele cha Watendakazi Bora Serikalini barani Afrika.
Tunzo hizo ziliandaliwa na Kampuni ya CEO Titans Building Nations ya Afrika Kusini, ambayo imejikita katika kutambua watu na viongozi wanaofanya kazi kwa ufanisi. 
Hafla ya kukabidhi tunzo hizo ilifanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Hilton jijini Nairobi, Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Dar es Salaam juzi jioni, mbali na Dk. Kamani, mwingine aliyepata tunzo hiyo ni Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu, aliyenyakua tunzo ya Uongozi Thabiti katika Vyombo vya Habari vya Tanzania.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tunzo hiyo, Dk. Kamani alisema hiyo ni ishara ya kuwa serikali na watendaji wa wizara yake wanawajibika kikamilifu.
Alisema wizara yake ina jukumu la kusimamia maendeleo ya mifugo, sekta ambayo imekuwa mkombozi mkubwa wa Watanzania wengi na kuwa, amefarijika kuona utendaji wa wizara yake ukitambulika kimataifa.
“Wakati naalikwa kuhudhuria hafla hii, nilijua ni masuala ya utendaji, sikufahamu kama kuna tukio hili la jitihada za wizara yangu kutambuliwa.
 “Nimefarijika kuona kazi yetu inatambulika, hivyo tutaendelea kuongeza bidii zaidi ili kutimiza azma yetu ya kuwainua wafugaji na wakulima kwa ujumla kiuchumi,” alisema Dk. Kamani.
Washiriki 100 kutoka taasisi mbalimbali barani Afrika walichaguliwa, ambapo wawakilishi 28 waliingia fainali kuwania tunzo katika nyanja tofauti.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru