Sunday, 10 August 2014

Bunge ladhibiti posho kwa wajumbe watoro

 • JUKATA laonya katiba si mradi binafsi
 • Mrema: Nina akili timamu sio za UKAWA

  NA WAANDISHI WETU
  BUNGE Maalum la Katiba limeweka udhibiti mkali kwa wajumbe wenye tabia ya kusaini posho bila kuhudhuria vikao.
  Wabunge wa bunge maalum la katiba wakiendelea na vikao
  Limesema kuwa lilishitukia mbinu hizo mapema kabla ya kuanza kwa vikao huku baadhi ya wajumbe wa kundi la Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa ndio wamekuwa na mchezo huo.
  Kutokana na hali hiyo, mfumo wa malipo kwa wajumbe kwa sasa umebadilika ili kuhakikisha wanaolipwa ni wale wanaostahili kwa maana ya kushiriki vikao vya bunge hilo.
  Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yusuph Khamis Hamad, alisema jana kuwa wajumbe ambao wamejisajili bila kushiriki vikao hawakulipwa na msimamo huo utaendelea.
  Awali, katika vikao vya bunge la katiba vilivyopita, utaratibu wa malipo uliwahusu wote ambao walijiandikisha, ambapo wengine walilipwa bila kuhudhuria baadhi ya vikao.
  Hamad alisema sasa wamedhibiti mchezo huo na kuwa utaratibu wa kuwalipa kwa wiki mbili kwa mkupuo, ambao ulitumika awali umesitishwa badala yake sasa malipo ni kwa wiki moja tu.
  "Tulishaona hiyo hatari mapema na kuamua kuchukua tahadhari na sasa mambo yanakwenda vizuri, wajumbe watakaokuja kujisajili tu kisha kutoweka, hawalipwi posho,” alisema.
  Akizungumzia kuhusu wajumbe wanaoingia kwa kofia ya ubunge wa bunge la Jamhuri, wanaotishiwa kufukuzwa na vyama vyao vinavyounda UKAWA, alisema kisheria mbunge huyo akivuliwa ubunge basi atapoteza sifa ya kuwa mujumbe wa bunge maalum la katiba.
  "Lakini sidhani kama mtu anaweza kuvuliwa ubunge kirahisi, kisa kafukuzwa na chama chake kwa kushiriki vikao vya bunge maalum, natumai hilo suala mahakama inaweza kuamua vizuri tu,na kusimamia haki," aliongeza.
  Alisema wajumbe wote wanaotoka katika UKAWA  ambao wamehudhuria vikao vya bunge hilo, wanaelewa kuhusu maslahi ya nchi kwanza, ni  wazalendo na hawapaswi kukashifiwa.  Mrema: Nina akili timamu

  Mbunge wa Vunjo, Agustino Mrema amewaeleza wananchi wake kuwa ana akili timamu na hawezi kususia vikao kama wajumbe wa UKAWA.
  Mrema, ambaye pia ni Mwenyekiti wa TLP, alisema jana kuwa kitendo cha UKAWA kususa bunge hilo ni kuwanyima haki za msingi za uwakilishi kwa wananchi waliowachagua.
  Alisema yeye amechaguliwa na wananchi wa Vunjo kwa ajili ya kuwatetea na kuwasemea matatizo yao, kama anavyofanya katika vikao mbalimbali vya bunge na sio kugomea vikao na kutoka nje.

  “Wapo watu wamekuwa wakinisema kuwa sifai kuwaongoza wananchi wangu, kwa sababu natumiwa na CCM kuwakandamiza ndio maana sijaungana na UKAWA, lakini najua hao wamekosa ya kusema,” alisema Mrema.  JUKATA laonya katiba si mradi
  Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limesema mchakato wa kuandika katiba mpya sio mradi wa mtu binafsi au chama chochote bali ni mradi endelevu wa watanzania wote.
  Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Deus Kibamba, aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini hapa kuhusiana na mchakato wa katiba.
  Kibamba alisema katiba mpya ya kidemokrasia na yenye viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Rais Jakaya kikwete wakati wa kuanzisha kwa mchakato huo ni muhimu kuzingatiwa.
  Alisema hakuna sababu ya kuharakisha kupatikana kwa katiba hiyo ili itumike katika uchaguzi mkuu ujao kwani muda uliobaki ni mfupi kukamilisha katiba.
  Aidha Kibamba alisema bado kunahitajika mazungumzo ya kina ili kufikia maridhiano kati ya UKAWA na bunge katika kuhakikisha katiba inapatikana.
  Alisema hivi sasa pamoja na kuendelea kwa juhudi mbalimbali bado UKAWA wameonyesha kutorejea na hivyo kuvitaka vyama hivyo kujali maslahi ya watanzania.
  Kwa mujibu wa Kibamba hivi sasa kuna mpasuko ndani ya UKAWA kwani, baadhi ya wabunge wanaoamini kuwa Bunge maalumu la katiba halipaswi kuendelea kwa sasa lakini pia wapo ambao wameona ni vyema kuhudhuria.

  "Haikuwa  kwa mashangao kushuhudia wajumbe watatu kutoka kundi la UKAWA wakitinga bungeni na kujiandikisha ili kuendelea na vikao," alisema.
   
   


   
   

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru