Wednesday 27 August 2014

Mzumbe waunga mkono Bunge la Katiba


NA WAANDISHI WETU
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Mzumbe, wameunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, wakisema wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mwenendo mzima wa Bunge hilo.
Pia wamesema mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya.
Wanafunzi hao walieleza msimamo wao juzi jioni chuoni hapo kwenye risala ambayo waliisoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete. Rais alitembelea chuo hicho ikiwa sehemu ya ziara yake mkoani Morogoro.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Boniface Juma, wanafunzi hao walisema ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.
Akijibu risala hiyo, Rais Kikwete aliwaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni, watumishi wengine wa chuo hicho na wanavijiji vya jirani na chuo kuwa: "Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama."
Aliongeza kuwa: ìNiliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa si Katiba ya CCM ama ya CHADEMA, ya NCCR au ya CUF. Niliwaambia hii ni Katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti.î
Kuhusu madai kuwa Rais Kikwete anakataa kukutana na wajumbe wa Bunge hilo ambalo wanaendelea kususia shughuli za Bunge hilo, alisema:  "Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.î
Hata hivyo, Rais Kikwete aliongeza kuwa ana matumaini mchakato huo utawwapatia Watanzania Katiba mpya. 
ìMimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri."

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru