Thursday 28 August 2014

Rushwa ya pilau, soda yawang’oa vigogo CHADEMA


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
MWENYEKITI wa CHADEMA wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Ernest Sheshe na viongozi wengine 10, wameachia ngazi kutokana na kuchukizwa na vitendo vya rushwa.
Sheshe na wenzake hao wamefikia uamuzi huo baada ya makada wengine kumwaga rushwa ya vyakula na vinywaji kwenye uchaguzi.
Makada wengi wa CHADEMA wamekuwa wakilalamika kuchezewa rafu na wapinzani wao, ambao wanatajwa kubebwa na baadhi ya viongozi wa makao makuu, ambapo vitendo vya rushwa vimetawala bila kukemewa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sheshe alisema ndani ya CHADEMA hakuna demokrasia na vitendo vya rushwa vinapewa kipaumbele.
Sheshe, ambaye alikuwa akitetea nafasi hiyo, alisema kabla ya kuanza kwa uchaguzi ngazi ya wilaya, wagombea walikuwa wakitoa rushwa na hata taarifa zilipofikishwa makao makuu, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, alituma waraka wa uchaguzi unaowataka viongozi wa mkoa na kanda kukemea vitendo vya rushwa, lakini hakuna kilichotekelezwa.

DK.SLAA
Alisema Katibu wa Kanda, Amani Golugwa, alishindwa kukemea rushwa hata za vyakula kwa kuwa wahusika ni wanaowaunga mkono.
“Wagombea wanagawa mpaka pilau na soda kwa wajumbe na viongozi wanaona ila hakuna hatua zinazochukuliwa kwa sababu ni watu wao. Unakaaje kwenye chama ambacho kimeshika hatamu kwa rushwa,” alisema Sheshe.
Pia alimrushia kombora, mgeni rasmi katika mkutano huo, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwa kushindwa kukemea wala kuchukua hatua dhidi ya rushwa hiyo.
Kwa upande wake, Lema alisema madai ya Sheshe ni kutapatapa na kuwa iwapo hakuridhika na matokeo, alipaswa kukata rufani na si kuhama.
Alisema wagombea wote waliridhika na matokeo hayo kasoro yeye na kwamba, chakula kilichotolewa kwenye mkutano huo kwa baadhi ya wajumbe ni fedha zilizochangwa na wajumbe wa mkutano huo.
“Chakula na vinywaji haikuwa rushwa ili mgombea fulani ashinde, bali kiliandaliwa kwa sababu wajumbe wasingeweza kukaa na njaa, aache umasikini,” alisema. 
Mkoani Tabora nako mambo si shwari kutokana na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa, Kansa Mbarouk, kujiengua ndani ya chama hicho.
Mbarouk alisema amechukua uamuzi huo kutokana na mambo kutokwenda vizuri huku akiwashushia lawama viongozi wa ngazi za juu kuvunja Kanuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru