Thursday, 28 August 2014

Wataka wadaiwa sugu wasakwe


Na Ahmed Makongo, Bunda
WADAU wa pamba katika wilaya ya Bunda, wamepitisha azimio la kuwasaka wakulima wanaodaiwa na kampuni zinazonunua zao hilo na kuwekeza katika kilimo cha mkataba wilayani hapa.
Azimio hilo lilipitishwa jana baada ya wadau hao kubaini kwamba wakulima wengi waliokopeshwa pembejeo na dawa za kunyunyizia pamba wilayani hapa, wanadaiwa mamilioni ya fedha.
Wadau hao wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Demunicus Lusasi, walipitisha azimio hilo katika kikao kilichoketi katika ukumbi wa Halmashauri mjini Bunda.
Katika kikao hicho wawakilishi wa kampuni hizo walilalamikia hali hiyo na kuitaka serikali kuingilia kati ili wakulima wanaodaiwa waweze kulipa madeni hayo kabla ya kuanza msimu wa kilimo wa mwaka 2014/1015.
Walisema kampuni zao ziliwekeza kwenye kilimo cha mkataba ili wakulima watakapovuna mazao yao walipe fedha hizo lakini, baadhi yao wameingia mitini na kukataa kulipa madeni yao.
Aidha, waliwalaumu baadhi ya wakulima am,bao baada ya kuvuna waliuza pamba kwenye kampuni zingine tofauti na makubaliano.
Kwa upande wake Mkaguzi wa pamba Mwandamizi wa Wilaya ya Bunda, Igoro Maronga, alisema kutokana na madai ya wanunuzi hao, kikao hicho kiliazimia kuwasaka wakulima ambao bado hawajalipa mikopo hiyo.
Maronga alizitaja baadhi ya kampuni zinazowadai wakulima hao kuwa ni pamoja na Oram inayodai  zaidi ya sh.milioni 23, S&C sh.milioni 60 na Birchard inayodai zaidi ya sh.milioni 50.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru