NA JANE MIHANJI, SONGEA
KAMPUNI ya uchimbaji makaa ya mawe ya TANCOAL, imesema
inalipa ushuru na mrabaha kwa serikali wa sh. bilioni mbili na kutoa asilimia
80 ya ajira kwa wazawa.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Mgodi wa Makaa
ya Mawe wa Ngaka, Tarn Brereton, alipokuwa akitoa maelezo ya maendeleo ya mgodi
huo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Alisema mbali na mrabaha, kampuni hiyo ambayo inaendeshwa
kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), imekuwa ikitoa zaidi ya sh.
milioni 600 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii katika kijiji cha Mbalawala
kilichoko karibu na mgodi huo.
“Fedha hizi tunazotoa kwa maendeleo ni sehemu ya faida tunayopata katika biashara ya makaa ya mawe ndani na nje ya nchi," alisema.
Brereton alisema fedha hizo zimesaidia katika kuwapatia
huduma ya maji, afya, shule na kuwawezesha vijana na kusaidia kikundi cha
maendeleo cha wanawake wanaotengeneza nishati hiyo kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani.
“Zaidi ya asilimia 80 ya watumishi ni kutoka mkoa wa Ruvuma, na kwa kufanya hivyo tunaendelea kutoa ajira kwa Watanzania,” alisema.
Makaa ya mawe ya Ngaka yanauzwa katika viwanda mbalimbali
vya kutengeneza saruji nchini, ikiwemo Tanga Cement, Lake Cement, Kiwanda cha Nguo
cha MELT, Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi, Mbeya Cement na SAJ Ceramic cha
Kenya.
Mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka una uwezo wa kuzalisha tani 480,000 kwa mwaka huku ukiwa na akiba ya
tani milioni 423 za makaa ya mawe.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru