Thursday, 7 August 2014

Mndolwa asema hana mpango na ubunge


NA MOHAMMED ISSA
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe Vijijini, Dk. Edmund Mndolwa, amesema hafanyi ziara kwa lengo la kutaka ubunge katika jimbo la Korogwe Vijijini.
Amesema anafanya kazi kama mjumbe wa NEC, kutoka wilaya hiyo na kwamba  lengo la ziara zake ni kukijenga Chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini  Dar es Salaam, jana, Dk. Mndolwa alisema hajawahi kufanya kampeni yoyote katika ziara zake hizo na kwamba lengo la ziara zake ni kuangalia uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alisema kila anapofanya ziara katika wilaya hiyo anafuatana na sekratieti ya CCM ya wilaya na amekuwa akimwalika Mbunge wa jimbo hilo, Stephen Ngonyani.
“Ziara zangu zina lenga kukijenga Chama chetu, sijawahi kufanya kampeni yoyote katika ziara zangu zote, kila ninapokuwa na ziara namualika mbunge wetu na ninakuwa na viongozi wa Chama wa wilaya,” alisema.
Alisema muda wa kufanya kampeni ndani ya Chama haujafika na viongozi wote waliochaguliwa wapo kihalali na anawaheshimu.
Dk. Mndolwa alisema mwaka 2010, aligombea ubunge katika jimbo hilo na akapata nafasi ya pili na kwamba alishiriki kumfanyia kampeni Ngonyani  bila kinyongo chochote.
“Sina kinyongo wala makundi niliposhindwa kwenye kura za maoni nilishiriki kumfanyia kampeni mbunge wa jimbo letu bila kinyongo,” alisema.
Alisema uhai wa Chama katika wilaya hiyo ni mzuri na hivi sasa wanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika badae mwaka huu.
Dk. Mndolwa alisema kuna kila sababu Chama kushinda katika uchaguzi wa serikali za mita na uchaguzi mkuu.
Alisema katika ziara zake hizo ametembelea kata 20, matawi 89 na kwamba kila tawi amekuwa akitoa ilani ya uchaguzi, kitabu cha maadili pamoja na bendera.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru