Thursday, 14 August 2014

Kigogo Maliasili aburutwa kortini


NA FURAHA OMARY
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imempandishwa kizimbani Ofisa Mhifadhi Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Richard Nchasi, kwa madai ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kwa kutoa hati za uwindaji wa wanyama.
Nchasi alifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na mashitaka manne ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri na kuisababishia wizara hiyo hasara ya dola za Marekani 1,860 (sh. 2,976,000).
Wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU, Leonard Swai, alimsomea  mashitaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Hassan.
Swai alidai tarehe tofauti kati ya Januari na Septemba, 2008, katika ofisi za wizara hiyo, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na cheo hicho, huku akijua na kwa nia ya kuidanganya wizara, aliandaa hati yenye namba 01235414 ya Agosti Mosi, 2008.
Inadaiwa hati hiyo ilikuwa inaonyesha kwamba Safari Club (T) Ltd, inatakiwa kulipa dola za Marekani 5,080 (zaidi y ash. milioni 8.5) ikiwa  ada ya uwindaji wa wanyama sita katika eneo la Kilwa South Mbemkulu, huku akijua si kweli.
Nchasi anadaiwa katika kipindi hicho aliandaa tena hati yenye namba 01235410 ya Februari 21, 2008, kuonyesha kwamba kampuni hiyo inatakiwa kulipa ada ya dola 6,580 (zaidi ya sh. milioni 11) ya uwindaji wa wanyama watano katika eneo hilo.
Ofisa Mhifadhi huyo anadaiwa katika kipindi hicho aliandaa tena hati yenye namba 01235415 ya Agosti Mosi, 2008, kuonyesha kampuni hiyo inatakiwa kulipa dola 6,335 (zaidi ya sh. milioni 10.6) ikiwa ada ya uwindaji ya wanyama saba kwenye eneo hilo.
Katika shitaka la nne, Nchasi anadaiwa katika kipindi hicho, jijini Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo, kwa kuelewa na kwa uzembe, aliisababishia wizara hiyo hasara ya dola 1,860 (zaidi ya sh. milioni 2.9) .
Mshitakiwa alikana mashitaka ambapo Wakili Swai alidai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya usikilizwaji wa awali na kwamba hana pingamizi juu ya dhamana.
Nchasi aliomba mahakama impatie dhamana, ambapo Hakimu Hassan alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka kutia saini bondi ya sh. milioni 10 na awe na wadhamini wawili wanaoaminika watakaotia saini bondi ya kiasi hicho.
Pia mmoja wa wadhamini hao awe na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani si chini ya sh. milioni 15 na mwingine atoke taasisi inayotambulika.
Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo alirudishwa rumande hadi Agosti 25, mwaka huu, kesi itakapokuja kwa usikilizwaji wa awali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru