Wednesday, 27 August 2014

Serikali kufuta ada sekondari  •  Lengo kuwa na elimu bure hadi kidato cha nne
  •  JK asema ni mkakati wa kuboresha elimu nchini  

NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza rasmi kuwa serikali inaangalia uwezekano wa kufuta ada katika shule zake za sekondari.
Hatua hiyo inalenga kuboresha Sera ya Elimu na kuhakikisha kila mwanafunzi anayeanza darasa kwanza anamaliza kidato cha nne.
Rais Kikwete alikuwa akizungumza jana na wanajumuia ya Chuo Kikuu  Mzumbe, Morogoro na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho ikiwa  sehemu ya ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20, mwaka huu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alitumia muda wa kutosha kuelezea historia ya maendeleo ya elimu nchini, mabadiliko ya mwelekeo wa elimu na sera ambazo zimeongoza mageuzi makubwa katika elimu chini ya uongozi wake.
Alisema serikali yake iliibua mpango wa ujenzi wa sekondari za kata ili kupanua wigo wa wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kada hiyo ya elimu kwa kuwa nafasi za wanafunzi kuingia sekondari zilikuwa finyu.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati anaingia madarakani mwaka 2005, wanafunzi waliokuwa wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa kati ya asilimia sita na 10 ya watoto wote waliokuwa wanamaliza elimu ya msingi. 
Alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata, ikiwa pamoja na kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni,  shule hizo zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio makubwa katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
Aliwaeleza mamia ya wanazuoni hao, watumishi wengine wa chuo na wananchi kuwa serikali wakati wote imekuwa inasaka kubuni sera za kuendeleza elimu na pia kuziboresha sera hizo.
ìKwa mfano sasa hivi tunaangalia jinsi gani ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za serikali kama namna ya kuhakikisha kila mtoto anayeanza darasa la kwanza anakuwa na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada,î alisema.
Aliongeza kuwa: ìTunaangalia kuondoa ada hii ambapo wazazi wanalipa sh. 20,000 kwa shule za kutwa na sh. 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila ya wasiwasi wa kukwamishwa na ada.î
Kuhusu historia ya kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alisema wakati serikali yake inaingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya.
ìKwa miaka mingi, hatukujenga shule mpya za sekondari, na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata.î
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zilikuwepo shule za sekondari 1,745 mwaka 2005 zikiwemo shule 1,202 za serikali na sasa ziko 4,576 zikiwemo shule 3,528 za serikali.
MAFANIKIO MAKUBWA 
Kuhusu maendeleo ya shule za kata, Rais Kikwete alisema zimekuwa na mafanikio makubwa kama ambavyo sekta nzima ya elimu imekuwa na mafanikio makubwa.
Rais Kikwete alielezea baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni upanuzi mkubwa wa elimu ya msingi na uandikishaji wa watoto kuingia shule, upanuzi wa elimu ya sekondari na ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari.
Pia alisema kumekuwa na upanuzi wa elimu ya juu ambapo sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma, ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka sh. bilioni 16 mwaka 2005 hadi kufikia sh. bilioni 345 kwa sasa, na kuongezeka kwa wakopaji kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi 95,000 katika kipindi hicho.
Rais Kikwete alisema kwa sasa serikali yake inapambana na changamoto zilizojitokeza kutokana na kupanuka kwa elimu nchini. 
Alisema moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo sasa imefikia kikomo kwa sababu, sasa wapo karibu wa kutosha kwa shule za sekondari zote nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru