Tuesday 26 August 2014

UVCCM yacharuka



NA WAANDISHI WETU
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Anthony Mavunde, amesema Tanzania haiwezi kuendeshwa na watu wanne wanaojiita viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kwamba hoja zao hazina mashiko.
Amewataka wananchi wasidanganyike na kukubali kushiriki katika maandamano yanayoandaliwa na viongozi hao kwa sababu hayana tija kwao na taifa kwa ujumla kwani yanalenga kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
Mavunde aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Mbagala Kiburugwa, Dar es Salaam, na kusisitiza kwamba matakwa ya UKAWA ya kutaka Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe,hayana nia njema na pia hawawezi kupewa nafasi ya kuipeleka nchi watakavyo.
Aidha aliwataka wananchi wasihofu juu ya upatikanaji wa katiba mpya kwa sababu itapatikana kwani bunge la katiba linaendelea na majadiliano na matakwa ya Watanzania yapo bungeni na si mitaani.
Alisema viongozi hao ni vigeugeu kwa sababu kila kukicha wanakuja na madai mapya, ambayo hayana tija kwa wananchi, hivyo aliviomba vyombo vya dola kuyasitisha maandamano waliyopanga kuyafanya.
Alisema wananchi wanatakiwa kuendelea kuipa ushirikiano CCM kwa sababu ndicho Chama pekee chenye kuweza kuwaletea maendeleo, tofauti na vingine ambavyo kazi yao kubwa ni kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Pwani, Mohammed Nyundo, aliwataka wananchi hao kutokubali ubabaishaji unaofanywa na viongozi wa upinzani kwa kuwa madhara yake ni makubwa.
Nyundo, ambaye pia ni MNEC kupitia wilaya ya Mafya, alisema CCM pekee ndicho Chama chenye uwezo wa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo na pia kinaendeleza amani na mshikamano kwa wote.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo aligawa kadi kwa wanachama wapya 213, wakiwemo 97 wa CCM na 116 wa UVCCM. Miongoni mwao wamo
wanne kutoka vyama vya Chadema na CUF.

Adam Said, ambaye alikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF wilaya ya Temeke, alisema sababu ya kukihama chama hicho ni baada ya kuchoshwa na ubabaishaji unaofanywa na viongozi, ikiwa ni pamoja na kutotekeleza ahadi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) Taifa, Mboni Mhita, alisema UKAWA, wanalipwa sh. 500,000 kutoka mataifa ya nje ili wavuruge mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Alisema kiasi hicho ni kikubwa kuliko wanacholipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, hivyo kwakuwa wanaangalia maslahi binafsi, ndio sababu hawataki kurudi kujadili mambo muhimu ya wananchi.
"Hawa UKAWA wanawadanganya wananchi kwani hawawaambii ukweli na ukweli ni kwamba wanalipwa fedha hizo kutoka nchi za nje, ambazo ni mara mbili ya wanazolipwa wajumbe wa bunge maalumu," alisema.
Mboni alisema kwenye rasimu inayojadiliwa bungeni, kuna mambo muhimu yanayohusu maisha ya Watanzania, lakini wao wanaangalia suala la uongozi pekee, kutokana na uroho wa madaraka.
Aliwahimiza  vijana na wanawake wenye sifa ya uongozi, kuchukua fomu na kugombania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2015.
Mboni alisema ni wakati wa makundi hayo kugombania nafasi katika uchaguzi huo badala ya kuwa washangiliaji kwani uongozi ni kupokezana kwa wenye sifa.
Wafuasi wa UKAWA walitoka katika Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (mjumbe wa bunge hilo) kuhitimisha kuchangia.
Katika mchango huo, alidai kuwa hawawezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.
Baada ya kauli hiyo, alitoka ndani ya Bunge hilo na kufuatiwa na Mwenyekiti wa UKAWA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wafuasi wao.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Jerry Silaa, amesisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi bado kina dhamira ya dhati ya kutaka katiba mpya, licha ya UKAWA kususia mchakato huo.
Alisema madai yanayotolewa na UKAWA kuwa CCM haina dhamira ya dhati ya kutaka katiba mpya, ni ya uzushi na yana lengo la kupotosha wananchi.
Aliongeza kuwa kitendo cha UKAWA kukimbia majadiliano katika bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma, kinatokana na umoja huo kuona kuwa hoja zao hazina mashiko kwa maslahi ya nchi.
Silaa, ambaye ni Meya wa Manispaa ya Ilala alisema ni lazima kila hoja ijadiliwe na kukubalika na sio kulazimisha kila hoja ikubalike pasipo kuwepo na mjadala.
Alisisitiza kuwa demokrasia ni maridhiano na sio kulazimisha hoja huku akiwataka UKAWA kurejea bungeni kwa majadiliano kama wana hoja za msingi.
Aidha, alisema serikali ya CCM itaendelea kuboresha maendeleo kwa wananchi bila kujali itikadi za kisiasa huku akiipongeza Halmashauri ya Kinondoni kwa kuanza mchakato wa ujenzi wa hospitali katika jimbo la Kawe.
Aliwataka vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali kama hatua ya kujikwamua kimaisha na  kutumia fursa ya upatikanaji wa mikopo inayotolewa na halmashauri mbalimbali nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru