Monday, 11 August 2014

Michezo Uhuru LEO!

Azam yaua Kagame

NA MWANDISHI WETU

TIMU ya Azam imetoa onyo kali kwa wapinzani kwenye michuano ya Kombe la Kagame, baada ya kuigagadua KMKM mabao 4-0.

Mchezo huo kwa pili kwa timu hizo tangu kuanza michuano hiyo juzi, ulichezwa jana kwenye Uwanja wa Amahoro, mjini Kigali, Rwanda.

Katika mchezo huo, Azam ilianza mchezo kwa kasi kwa kusaka mabao ya mapema.

Azam ilipata bao la kwanza sekunde ya 58 kupitia kwa John Bocco, akiunganisha pasi safi iliyopigwa na beki Shomari Kapombe.

Dakika ya nne Azam kupitia kwa Bocco nusura ipate bao baada ya kuachia shuti kali kabla ya kipa wa KMKM kupangua mpira huo.

Azam iliendelea kufanya mashambulizi makali langoni mwa KMKM ikitafuta mabao zaidi.  Dakika ya 16 Saint Lionel aliipatia timu yake bao la pili akiunganisha mpira wa adhabu ndogo.

Dakika ya 29 Lionel alipachika bao la tatu, baada ya kuwatoka mabeki wa KMKM na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Dakika ya 52 Bocco alifunga bao la nne baada ya kupata pasi ya Kapombe baada ya kuwazidi mbio mabeki wa KMKM.

Hata hivyo, KMKM nayo ilijizatiti na kujaribu kutafuta bao la kufutia machozi ambapo dakika ya 56 ilipata nafasi kabla ya beki Aggrey Morris kuokoa hatari.

Azam imefikisha pointi nne baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu na wenyeji Rayon Sports ya Rwanda.

Timu hiyo inashiriki michuano hiyo kuchukua nafasi ya Yanga iliyoenguliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).


 KimataifaLONDON, England

TIMU ya Arsenal imetwaa ubingwa wa Ngao ya Hisani, baada ya kuizabua Manchester City mabao 2-0 katika mchezo mkali kwenye Uwanja wa Wembley, London.

Mchezo huo ulikuwa ni maandalizi ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu England utakaoanza Agosti 16, mwaka huu.

Arsenal ilipata bao la kwanza dakika ya 21 lililofungwa na Santi Cazorla, kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Timu hiyo iliongeza kasi ya mchezo na kuwabana mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, baada ya kucheza mpira wa kushambulia.

Arsenal ilipata bao la pili dakika ya 42 lililofungwa na mchezaji, Aaron Ramsey, kufuatia kazi nzuri na Yaya Sanogo na Dedryck Boyata.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru