SERIKALI imewaagiza viongozi wa wilaya ya Mvomero na mkoa wa Morogoro kukaa pamoja kujadili tatizo la wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kushindwa kumaliza kidato cha nne kwa idadi ile ile.
Agizo hilo lilitolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akiwahutubia wananchi wa kata ya Kibati, wilayani Mvomero akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.
Rais Kikwete alisema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kuwa wanafunzi 3,060 kati ya 5,255 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2009, walishindwa kumaliza kidato cha nne mwaka jana.
Alisema idadi hiyo inamaanisha kuwa ni asilimia 42 tu ya wanafunzi hao ndio waliweza kumaliza kidato cha nne huku asilimia 58 wakishindwa kuhitimu elimu hiyo.
“Kaeni mtafakari juu ya tatizo hilo mjue nini cha kufanya, ni kwa nini wanafunzi hao wanashindwa kumaliza shule kama walivyoanza, wanaishia na wapi,” alisema.
Rais aliahidi kuwapatia sh.milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana la shule ya sekondari ya Nguru iliyoko kata ya Kibati wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, alipoulizwa juu ya tatizo hilo, alisema kuna sababu nyingi zinazochangia hilo, ikiwemo wafugaji kuhama na familia zao.
Sababu nyingine, kwa mujibu wa Mtaka, ni wazazi kuamua kuwapeleka watoto shule za binafsi, hivyo kufanya idadi ya watoto waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kwenye shule za serikali kupungua.
Aidha, alisema baadhi ya wazazi hawana uwezo hivyo kushindwa kuwaendeleza watoto wao ikiwemo kuwasimamia kitaaluma.
“Idadi kamili ya watoto wanaochanguliwa na kujiunga kidato cha kwanza haiwezi kuwa sawa kutokana na sababu hizo.
“Tumekuwa tukifutilia wanafunzi ambao hawaendi shule na badala yake wanafanya kazi za ndani, tunawarejesha shuleni na kuwachukulia hatua wazazi wao,” alisema.
Hata hivyo, alisema Baraza la Madiwani katika halmashauri ya wilaya hiyo liliridhia watoto wote wanaochanguliwa kuingia kidato cha kwanza wapokelewe bila kujali ada na michango mingine.
Pia alisema mikakati mingine wanayofanya ili kukabiliana na tatizo hilo ni kuhimiza ujenzi wa mabweni na kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa sekondari zote.
Thursday, 28 August 2014
Kikwete atoa agizo zito Morogoro
02:38
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru