Thursday, 28 August 2014

Sekretarieti ya Ajira yawananga wasomi

  • Yasema wengi wanawasilisha nyaraka duni
  •  Wengine wamesoma vyuo visivyotambuliwa 
Na Mwandishi Wetu
WAHITIMU wengi wanaotuma maombi ya kazi serikalini hawajui taratibu za kufuata, hivyo kushindwa kunufaika na fursa hizo kutokana na kuwasilisha nyaraka zisizokithi vigezo, imeelezwa.
Pia baadhi ya waombaji hao wamekuwa wakiwasilisha vyeti vya elimu visivyokidhi viwango na wengine kusoma katika vyuo ambavyo havitambuliki na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kutokana na sababu hizo, baadhi ya wadau wamekuwa wakiitupia lawama serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kuwa imekuwa ikifanya upendeleo katika utoaji wa ajira kwa kushindwa kuwaita kwenye usaili walioshindwa kukidhi viwango mapema.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar er Salaam, jana, Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira,
Bi.Riziki Abraham
Riziki Abraham, alisema baadhi ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha nyaraka za kupotelewa na vyeti vya shule badala ya vyeti vya taaluma.
Alisema idadi kubwa ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha barua kutoka Jeshi la Polisi kuonyesha wamepotelewa vyeti hivyo ama kuharibika, jambo ambalo si sahihi.
Pia alisema baadhi ya waombaji hususan wa vyuo vya nje, wamekuwa wakiwasilisha vyeti vya taaluma visivyo na vigezo kumwezesha mhusika kupata ajira nchini.
Kutokana na matatizo hayo, serikali imewataka waombaji wenye matatizo katika vyeti vyao vya taaluma na taarifa zingine muhimu, kuwasiliana na mamlaka husika kwa msaada zaidi.
Wahitimu waliopoteza vyeti
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imewataka wahitimu waliopoteza, kuibiwa ama kuharibikiwa na vyeti vya taaluma, kutoa taarifa polisi kisha kuwasilisha taarifa hizo katika mamlaka zinazohusika kama Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kwa vyeti vya kidato cha nne na sita.
Kwa vyeti vya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na elimu ya juu ni TCU ili waweze kuelekezwa taratibu za kufuata ikiwamo kutangaza kwenye vyombo vya habari.
Hatua hiyo inalenga kumwezesha mhusika kupata vyeti vingine huku taarifa zake za kupotelewa zikiwasilishwa Sekretarieti ya Ajira kwa wakati.
Waombaji waliosoma nje
Wahitimu waliosoma nje ya nchi iwe ngazi ya sekondari ama vyuo vikuu, wanatakiwa kuwasilisha taarifa pamoja na vyeti vyao kwa mamlaka husika ili kuhakikiwa na kupewa barua za uthibitisho kuwa vyuo walivyosoma vinatambulika ama la.
Taarifa hizo zinapaswa kuwasilishwa NECTA, VETA, NACTE na TCU, ambazo ndizo zenye mamlaka ya kuthibitisha na kuwasilisha taarifa za mhusika katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira.
Utaratibu wa mwombaji kuwasilisha taarifa za kupotelewa vyeti kuwasilisha utambulisho wa matokeo ama nyaraka pindi anapoomba ajira, haukubaliki.
Wenye majina tofauti 
Kumekuwepo na baadhi ya watu kubadilisha majina kwa kutotumia ya utotoni, kubadili dini, kutumia ubini wa mume hali, ambayo imechangia kuwa na majina tofauti na cheti za kuzaliwa.
Kutokana na hilo, wanatakiwa kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuwasilisha maombi ya kazi kwa Sekretarieti ya Ajira.
Mikataba ya ajira kwa wastaafu
Abraham alisema kuwa serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuzuia wastaafu kuongezwa mikataba ya ajira ili kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini kupata ajira.
Alisema kwa sasa wastaafu waliopewa mikataba ya ajira serikalini ni asilimia 0.1 na kwamba, hilo limetokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete.
“Rais Kikwete aliagiza kupunguzwa kwa mikataba ya watumishi wa serikali waliostaafu ili kutoa fursa kwa vijana wapya kuingia kazini. Agizo hilo limeendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa na limepungua,” alisema.
Pia, alisema sekretarieti imeanza utaratibu wa kufanya makongamano katika vyuo mbalimbali  kuhamasisha vijana kuwa na mawazo ya ujasiriamali ili kujiajiri kwani fursa ya ajira ni ndogo nchini.
“Tunawataka pia kujitahidi kufanya vizuri katika masomo yao kwani, tunatarajia kuanza utaratibu mpya wa kuangalia viwango vya ufaulu,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru