Thursday, 21 August 2014

Msimamo mzito Kamati Kuu CCM  • Bunge la Katiba mbele kwa mbele, mchakato safi
  • CC yawaengua mawaziri safari za JK nje ya nchi
  • Yatoa maagizo mazito kwa mawaziri na wabunge

Na Happiness Mtweve, Dodoma
KAMATI Kuu ya CCM, imewaagiza mawaziri, manaibu mawaziri na wabunge wasiohudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kuhudhuria mara moja.
Imesema mchango wa mawaziri na wabunge katika Bunge hilo ni muhimu ili kuhakikisha Katiba bora ya wananchi na yenye maoni ya wengi inapatikana.
Kutokana na hilo, imetangaza kupunguza idadi ya mawaziri na manaibu mawaziri ambao kisheria ni wajumbe wa Bunge hilo, kuongozana na Rais Jakaya Kikwete katika ziara zake nje ya nchi.
Imesema kuanzia sasa Rais Kikwete ataongozana na idadi ndogo ya mawaziri pale inapobidi kwenye msafara wake katika shughuli mbalimbali.
Agizo hilo la Kamati Kuu ya CCM, ambayo likutana juzi chini ya Rais Kikwete, huenda linatokana na baadhi ya mawaziri kulalamikiwa kutohudhuria vikao vya bunge hilo. 
Hata hivyo, wengi wamekuwa wakishindwa kuhudhuria baadhi ya vikao kutokana kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, kuhusiana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo ni miongoni mwa mambo yaliyoazimiwa katika kikao hicho.
Nape alisema Kamati Kuu imesema inapenda kuona mchakato wa Katiba Mpya ukikamilika kwa wakati ili kutoa fursa ya kuendelea kwa mambo mengine kwa maendeleo ya taifa.
“Tunachokihitaji hapa ni kuhakikisha tunamaliza jambo hilo lililopo mbele yetu na kuendelea na mambo mengine,” alisema Nape.
Nape aliongeza kuwa katika kikao hicho, Kamati Kuu imeridhishwa na majadiliano yanayoendelea katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba pamoja na upigaji kura.
Pia alisema kuwa wajumbe wote wametakiwa kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki kwenye mijadala kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele ili kutimiza malengo ya watanzania ya kuwa na katiba bora.
“Kamati Kuu imeridhishwa na namna wajumbe wanavyoshiriki mijadala na kujenga hoja, pia wanavyoshughulikia mitazamo tofauti katika majadiliano yao na upigaji kura,” alisema Nape.
Alisema Kamati Kuu pia imemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulaharman Kinana, kuendelea kukutana na kufanya majadiliano na vyama vya siasa vilivyokuwa katika mazungumzo ya maridhiano chini usimamizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa. 
Hata hivyo, majadiliano hayo yalivunjika kutokana na kushindwa kufikiwa kwa makubaliano kutokana na kila upande kushindwa kukubaliana na hoja za mwingine.
Mazungumzo hayo yanahusisha vyama vya CCM, CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi.
Kuhusu jitihada zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Nape alisema Kamati Kuu imepongeza ushiriki wa CCM na vyama vingine ambavyo ni wanachama wa TCD, katika juhudi zinazolenga kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana.
“Kamati Kuu inaendelea kuwasii Watanzania kuendelea kushikamana na kuvumiliana, pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja za Katiba kwani, amani na utulivu ni muhimu kuliko tofauti zetu za kimtazamo,” alisema Nape.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru