Thursday, 28 August 2014

Vyama vya siasa vyatakiwa kuweka utaifa mbele

  • Vyaonywa maslahi ya vyama yataiweka nchi pabaya
NA KHADIJA MUSSA
VIONGOZI wa vyama vya siasa watakaokwenda kukutana na Rais Jakaya Kikwete, wametakiwa kuweka mbele masuala yanayohusu taifa na si misimamo binafsi ya vyama vyao.
Aidha wasomi nchini wamempongeza Rais Kikwete kwa kukubali kukutana na viongozi wa vyamaa hivyo vya siasa kwa kuwa ni ishara nzuri kwa kiongozi wa nchi kutokuwa na ubaguzi hata kwa watu wasiomuunga mkono.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Rais Kikwete kukubali kukutana na viongozi wa vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Viongozi hao waliazimia kutafuta nafasi ya kukutana na Rais Kikwete kwa lengo la kushauriana naye kuhusu mambo mbalimbali, ukiwemo mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, unaoendelea mjini Dodoma. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
TCD inaundwa na vyama vyenye uwakilishi bungeni, ambavyo ni CCM, CUF, CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na UDP. Mwenyekiti wa sasa wa TCD ni
MH.John Cheyo
John Cheyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda, alisema ni vyema viongozi hao wa vyama vya siasa watakapokwenda kukutana na Rais Kikwete, wabebe maslahi ya taifa na si ya vyama.
Mwakagenda alisema viongozi hao wanapaswa kuweka kando misimamo ya vyama vyao na badala yake waungane pamoja na kwenda kujadili masuala yanayohusu taifa.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya JUKATA, George Mollel, amesema hakuna sababu ya kufanyika kwa maandamano ya kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu hayana faida, badala yake watu wengi wasiokuwa na hatia wataumia na wengine kupoteza maisha.
Mollel alisema jana kuwa, badala ya kufanyika kwa maandamano, wanaotaka kuyafanya watumie hoja katika kupinga kuendelea kwa vikao hivyo.
Hivi karibuni, viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walitangaza kuitisha maandamano nchi nzima kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, amempongeza Raisk Kikwete kwa kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini.
Dk. Bana alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, hiyo ni ishara tosha kuwa kiongozi huyo wa nchi hana ubaguzi na ni karama aliyojaaliwa na Mola ya kumsikiliza kila mtu.
Msomi huyo alisema anaamini kikao hicho kitasaidia kufikiwa kwa muafaka iwapo viongozi hao wa kisiasa watakuwa na hoja kwa sababu Bunge walilogomea kushiriki baadhi ya vyama, lipo kwa mujibu wa sheria na Rais yupo kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, alisema amefurahishwa na hatua ya Rais ya kukubali kukutana na viongozi hao kwa sababu ameonyesha kuwa ni muungwana na ana dhamira ya dhati ya kutaka maridhiano yafikiwe na hatimaye katiba mpya ipatikane.
Hata hivyo, Mhadhili huyo alitoa ombi kwa UKAWA, ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo vizuri na hatimaye maridhiano yapatikane, lengo likiwa ni kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana na mwisho wa siku wasije wakadai kuwa Rais amevuruga mchakato huo.
Wafuasi wa UKAWA walitoka nje Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (mjumbe wa bunge hilo) kuhitimisha kuchangia. Katika mchango wake, Lipumba alidai hawawezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.
Baada ya kauli hiyo, Lipumba aliotoka ndani ya Bunge hilo, akifuatiwa na Mwenyekiti wa UKAWA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wafuasi wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru