Wednesday, 13 August 2014

Serikali yaongeza nguvu kuikabili Ebola



  •  Yatenga sh. bilioni 1.8 kupambana nayo 

NA RABIA BAKARI
SERIKALI imeendelea kuchukua tahadhari kutokana na ugonjwa wa Ebola kusambaa kwa kasi kubwa na kubisha hodi katika nchi za Afrika Mashariki.
Ugonjwa huo ambao uliweka mizizi katika nchi za Afrika Magharibi, umeua mamia ya watu na kasi yake imezidi kuyatisha mataifa mbalimbali duniani.
Kutokana na tishio hilo, serikali imefunga vifaa vya kisasa katika viwanja vikubwa vya ndege nchini ili kudhibiti ugonjwa huo kuingia.
Tayari mashine maalumu zimefungwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kubaini wageni wenye vimelea hivyo huku wataalamu wa afya wakifanya ukaguzi.
Pia imetenga vyumba maalumu kwenye viwanja vya ndege nchini vyenye wataalamu na vifaa vya kisasa, ili kuwafanyia uchunguzi wageni na watu mbalimbali watakaoonekana kuwa na vimelea vya Ebola.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashidi, alisema jana kuwa serikali imetenga sh. bilioni 1.8 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) na wadau wengine duniani,  walikutana kujadili tishio la kusambaa kwa ugonjwa huo. Katika mkutano huo, alisema  walikubaliana kila nchi kutumia fedha zake za ndani badala ya kusubiri za wafadhili.
HALI YA EBOLA
Dk. Seif alisema Machi, mwaka huu, serikali ilipokea taarifa kutoka WHO kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo ulioanzia Guinea na kusambaa katika nchi zingine za Sierra Leone, Liberia na Nigeria.
Hadi Agosti 6, mwaka huu, idadi ya watu waliougua walikuwa 1,779 na waliopoteza maisha ni 961.
Hata hivyo, alisema tangu kubainika kwa ugonjwa huo, serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ili kudhibiti na mpaka sasa hakuna mgonjwa wala anayehisiwa kuwa na vimelea vyake.
Alisema njia za kukabiliana na ugonjwa huo ni kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mwathirika.
“Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa kwa dalili hizo, wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu, kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya pale mtu anapohisi kuwa na dalili za ugonjwa huo,” alisema.
Dk. Seif alisema dalila za ugonjwa wa Ebola ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu misuli, kuumwa na kichwa na kutokwa vidonda kooni.
Dalili zingine ni kutapika, kuharisha, kutokwa vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na baadhi ya wagonjwa hutokwa damu ndani na nje ya mwili. Dalili zake huonekana kuanzia siku mbili hadi 21.
Ugonjwa wa Ebola hauna tiba maalumu wala chanjo, licha ya kuwa mgonjwa hutibiwa kwa kutegemea dalili atakazokuwa nazo.
Alisema mapambano dhidi ya ugonjwa huo si ya serikali pekee, bali kila mmoja kwa nafasi yake achukue jukumu ili kuepusha taifa kuingia katika janga hilo. 
MIKAKATI YA KUDHIBITI
Mganga Mkuu wa  Serikali, Dk. Donan Mmbando, alisema mikakati iliyopo ni kuongeza wahudumu wa afya na wataalam wa sekta hiyo kwa wingi zaidi tofauti na sasa.
Pia alisema vyumba vilivyotengewa kwenye viwanja vya ndege vikubwa nchini, vina wataalamu wa kutosha kuwahudumia watu wenye viasharia vya ugonjwa huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru