Thursday, 14 August 2014

Kibonde, Gardner wapandishwa kizimbani


NA JESSICA KILEO
WATANGAZAJI wawili, akiwemo Ephraim Kibonde wa Kituo cha Redio cha Clouds, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu mashitaka mawili, likiwemo la kumtukana ofisa wa polisi.
Kibonde (42) na Gardner Habash (41), walifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mfawidhi, Anicieta Wambura.


Wakili wa Serikali Salum Ahamed, alidai kuwa Agosti 9, mwaka huu, katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, wilayani Kinondoni, washitakiwa walimtukana tusi la nguoni ofisa wa polisi kituoni hapo mwenye namba E 884 SGT, Silivester.
Kibonde, anadaiwa siku hiyo katika maeneo ya Bamaga, alikataa kutii amri halali aliyopewa na polisi ya kutakiwa kurudisha gari eneo la tukio baada ya ajali.
Ilidaiwa mshitakiwa alikataa kutii amri hiyo, badala yake alikimbiza gari hadi alipokamatwa eneo la Ubungo kwenye mataa.
Washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Septemba 10, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Walipewa dhamana baada ya kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili, waliotia saini bondi ya sh.500,000 kila mmoja.
Baada ya hapo, Kibonde alipandishwa kizimbani tena mbele ya hakimu huyo, akikabiliwa na mashitaka mawili ya kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa.
Wakili Ahmed alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9, mwaka huu, maeneo ya Makumbusho, barabara ya Bagamoyo.
Alidai mshitakiwa alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T.759 CPM aina ya Toyota kwenye barabara ya umma akiwa katika hali ya ulevi kwa kipimo kilichopindukia cha ML 190.9.
Pia Kibonde alidaiwa katika eneo hilo, alikuwa akiendesha kizembe gari huku akishindwa kuacha nafasi kwa magari mengine na kugonga gari lenye namba za usajili T.960 CBB aina ya Hyundai Tucon.
Wakili huyo alidai tukio hilo lilisababisha uharibifu wa gari la mshitakiwa na lingine lenye namba za usajili T.960.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Septemba 9, mwaka huu, kesi itakapotajwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliotia saini bondi ya sh.milioni nne kila mmoja.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru