Thursday, 7 August 2014

Kinana: Tutazidi kulinda maslahi ya wafanyakazi


NA WAANDISHI WETU, DODOMA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abrahaman Kinana, amesema Chama kitaendelea kuwa karibu na wafanyakazi katika kuhakikisha maslahi yao yanapatikana. .
Kinana alisema hayo jana alipokuwa akipokea kadi ya uanachama kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hotelini, Nyumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU) katika ukumbi wa CCM Makao Makuu, mjini hapa.
Alisema mara nyingi wafanyakazi wamekuwa wakijitetea wenyewe lakini kwa sasa kutokana na kupokea kadi hiyo kunakifanya chama kuwa karibu zaidi na wafanyakazi.
Kinana alisema CCM ni chama cha  wakulima na wafanyakazi lakini kimekuwa hakipo karibu sana na wafanyakazi ila kimekuwa karibu na serikali.
“Nadhani Chama kina wajibu wa kuwa karibu na wafanyakazi kuangalia maslahi yao, haki mazingira na kuwasemea,‘’ alisema.
Alisema wakati mwingine Chama kimetakiwa kuwa kipaza sauti cha wafanyakazi na haiwezekani kufanya vyote hivyo bila ya kuwa sehemu ya wafanyakazi.
Kinana alisema Chama pamoja na yeye binafsi atahakikisha anakuwa karibu na CHODAWU na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ili kuwa karibu na wafanyakazi  katika maeneo yao kwa kuwa wamekuwa na malalamiko mengi.
Kwa mujibu wa Kinana alisema tangu kuchaguliwa kuwa Katibu mkuu amekuwa  karibu sana na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa sababu walimwandikia  barua kumwalika.
Alisema alishawahi kufanya vikao vingi nao na kila akienda  katika ziara zake anakutana na makundi mbalimbali kuzungumza nao wakiwemo walimu.
Alisema ni wajibu wa CCM sasa kama watendaji kuwa wanachama wa chama cha wafanyakazi kupitia sehemu inayowahusu na miezi michache ijayo ataanzisha tawi la chama hicho katika ofisi za CCM Makao Makuu ili wafanyakazi wapate chombo husika cha kupigania haki zao.
“Dhamira yangu ni kumfanya kila mtumishi wa Chama ambaye ataridhia kwa hiyari yake kuwa mwanachama wa CHODAWU na nina hakika watapenda,’’ alisema
Alisema kwa kuanzia ni vyema  kuanzishwa kwa tawi la Chama hicho katika Ofisi Kuu ya CCM na kuhaidi kuwa mmoja wa waanzilishi mpaka watakapopatikana viongozi watakaochaguliwa kwa njia ya  demokrasia.
“Tutaangalia muundo wa matawi yetu maana yametapakaa nchi nzima maana wanachama wana malalamiko yao lakini sina uhakika kama wanamahali pazuri pa kusemea,nimekuwa nikipokea barua watu wanalalamika kupitia chombo fulani sasa mdomo wa wengi ni bora kuliko wa mmoja mmoja,” aliongeza Kinana.
Aidha alisema anajivunia kuwa mwanachama wa CHODAWU kwa kuwa hajawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha wafanyakazi.
“Mimi  kwa kipindi kirefu nimekuwa jeshini, na jeshini kama mnavyojua ni amri tu na hutakiwi kuwa na mwanachama wa chama chochote,” alisema Kinana.
Kinana alitumia nafasi hiyo kumpongeza rais mpya wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Gratian Mukoba na kuahidi kutoa ushirikiano.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru