Na Ahmed Makongo, Bunda
WAKULIMA walioko kwenye vikundi vinavyowezeshwa na Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo Wilayani (DASIP) wilayani Bunda, wameupongeza mpango huo kwa uwainua kiuchumi.
Baadhi ya wakulima hao waliipongeza DASIP kwa kusaidia kuinua maisha yao tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Wakiongozwa na mkulima bora wa mkoa wa Mara, Mugole Lusungura, walisema kabla ya mradi huo kuanza, walikuwa na maisha duni ikilinganishwa na sasa.
“Kabla ya DASIP, maisha yetu yalikuwa dunia lakini baada ya kupata mafunzo kupitia mashamba darasa tumepata maendeleo makubwa mno. Binafsi nimejenga nyumba, nimenunua mifugo na ninasomesha watoto kutokana na kilimo,” alisema Lusungura.
Lusungura alisema kupitia mradi huo, pamoja na elimu waliyopewa ya kilimo cha tija, kwa sasa wanazalisha mazao mengi yanayoinua kipato cha wakulima wengi wanaozingatia sheria na kanuni za kilimo bora.
Kwa niaba ya wenzake alipongeza mafunzo hayo yaliyoendeshwa kupitia shamba darasa la Shule ya Msingi Kinyambwiga, wilayani humo na kusema yamekuwa yakiwaongezea uwezo.
Aidha, wakulima hao waliipongeza serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao umewainua kiuchumi na kwamba miradi mingine ya kuendeleza wakulima iendelee kuletwa kwa sababu kilimo ndicho kinachoweza kuwainua watu wa vijijini.
Mratibu wa DASIP Wilaya ya Bunda, Blasius Ogola, alisema mradi huo umewawezesha wakulima wengi wilayani humo kujiinua kiuchumi na kupata maendeleo.
Ogola alisema DASIP imekuwa ikiwawezesha wakulima kupitia mashamba darasa, ili kuwajengea uwezo wa kulima kilimo chenye tija ambacho kitawaletea maendeleo.
Thursday, 28 August 2014
Wapongeza DASIP kuwatoa kimasomaso
02:45
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru