Thursday, 14 August 2014

Shibuda: Fikra za UKAWA ni chakavu



  • Sitta awapuuza, asema Bunge litaendelea
  • Wasomi wawashangaa, wawaonya wananchi

NA WAANDISHI WETU, DODOMA
MAMBO yanazidi kwenda mrama kwa viongozi wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutokana na kuendelea kuvurumishiwa makombora kutokana na kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.

Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, amesema kundi hilo lina fikra chakavu na ndiyo sababu amewazidi uwezo wa kufikiri na kuamua kurejea kushiriki vikao vya bunge hilo.
Shibuda, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alitangaza kutogombea tena ubunge kupitia CHADEMA, alisema jana kuwa viongozi wa UKAWA hawana nia njema na Watanzania hivyo, watu wenye busara na wanaojali maslahi ya umma hawawezi kugoma.
Alikuwa akizungumza jana katika Viwanja vya Bunge, alipowasindikiza wafugaji kutoka mikoa mbalimbali kuonana na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.
“Hata wanasayansi hutofautiana kimawazo, lakini mwisho wa siku hukaa pamoja na kugundua kitu kipya. Ingekuwa vinginevyo tusingekuwa na Paracetamol leo,” alisema na kuongeza: “Hawa wenzangu lengo kubwa ni kugawana madaraka, mimi nataka Katiba bora ya Watanzania si madaraka.”
Alisema kundi hilo ni watu wenye sera ya maisha  ya anasa ndiyo maana  hakuna mkulima wala mfugaji ambaye ni mjumbe wa kundi hilo.
‘’Haiwezekani watu wanaotofautiana kimawazo kugeuka kuwa chinjachinja. Tunataka viongozi ambao wanakabiliana na matatizo ya wananchi na si kukimbia matatizo,’’ aliongeza.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa wafugaji na wakulima kutokubali kutumiwa na wanasiasa wanaotaka kujikwezwa kwa kutumia mchakato wa Katiba.
Pia amemtaka Sitta kutotishika na kauli za kundi hilo kwa kuwa  wananchi wanachohitaji ni Katiba inayogusa matatizo yao na si vitisho vya watu wasiokuwa na tija.
Kwa upande wake, Sitta alisema Bunge lipo kwa mujibu wa sheria na litaendelea na kazi zake kama kawaida na Watanzania watarajie Katiba bora.
‘’Tupo ndani ya Bunge na tunatosha na wakati wa kupata katiba mpya ni sasa na kidemokrasia ya kura za wengi ndio itakazotoa Katiba, sisi wenye uzalendo tutahangaika nayo mpaka ipatikane,’’ alisema.
Alisema mchakato wa Katiba unahusu wananchi wote bila kujali chama wala kabila na kikubwa ni kuwepo kwa haki za raia.
‘JK wapuuze UKAWA’
Wakati Shibuda akisema hayo, Mwenyekiti wa Tanzania Kwanza, Augostino Matefa, amemshauri Rais Jakaya Kikwete kuwapuuza UKAWA na kuacha Bunge liendelee na vikao vyake.
Alisema madai ya UKAWA hayana msingi wala maslahi kwa taifa na kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya unapaswa kuendelea kama kawaida.
Matefa alitoa kauli hiyo siku moja baada ya viongozi wa UKAWA kutoa masharti mapya kwa Rais Kikwete, wakimshauri kusitisha vikao vya bunge hilo vyinginevyo wataingia mtaani kufanya maandamano.
Juzi, viongozi wa UKAWA, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (CHADEMA) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), walisema watawaongoza na kuwashawishi wananchi nchini kote kuingia barabarani.
Matefa alisema viongozi wa UKAWA, hawalitakii mema taifa na iwapo Rais Kikwete atawasikiliza, atakuwa hajawatendea haki Watanzania.
“Tunaamini Rais wetu hawezi kusikiliza maneno yasiyo na  kichwa wala miguu yaliyotolewa na UKAWA na iwapo atawasikiliza atakuwa hajawatendea haki Watanzania walio wengi,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru